Cisse azidi kujisafishia CV

Muktasari:

Cisse ndiye alikuwa nahodha wa Senegal wakati walipofuzu kwa mara ya kwanza kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 ambapo walifika robo fainali.

Moscow, Russia. Kocha Aliou Cisse wa Senegal, amezidi kujisafishia jina kwa kuwa kocha wa kwanza kupata ushindi kati ya makocha wa timu tano zinazoliwakilisha bara la Afrika katika fainali za Kombe la Dunia 2018.

Cisse ndiye alikuwa nahodha wa Senegal wakati walipofuzu kwa mara ya kwanza kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 ambapo walifika robo fainali.

Enzi zake Cisse alikuwa mlinzi wa pembeni kulia alikua maarufu mno miongoni mwa mashabiki wengi wa soka nchini Uingereza kutokana  na makeke yake.

Cisse mwenye miaka 42, amesifiwa na wachambuzi wa soka wakisema amethibitisha kuwa kazi ya ukocha licha ya kusomea lakini kwa watu waliocheza soka wanakua na mafanikio zaidi wanapogeukia ukocha.

Uchezaji wake wa kibabe akiwa mlinzi wa pembeni kulia ulimfanya atimuliwe na timu yake ya Birmingham kwenye Ligi ya England, baada ya kuonyeshwa kadi nyingi za njano.