Bondia Katie Taylor kutetea taji WBA kwa wanawake

Muktasari:

Kabla ya kujitosa kwenye ngumi za kulipwa Katie Taylor alikuwa bingwa wa Olimpiki uzani wa light alioutwaa kwenye michezo ya mwaka 2012.

London, England. Bondia wa Katie Taylor mzaliwa wa Ireland, atatetea taji lake la ubingwa wa Dunia wa vyama vya IBF na WBA uzani wa Light kwa wanawake kwa kucheza na Cindy Serrano, pambano litakalofanyika mjini Boston, Oktoba 20 mwaka huu.

Kabla ya kujitosa kwenye ngumi za kulipwa Katie Taylor alikuwa bingwa wa Olimpiki uzani wa light alioutwaa kwenye michezo ya mwaka 2012.

Bondia huyu alitetea ubingwa wa Dunia mwezi uliopita alipomkalisha Kimberly Connor kwa KO raundi ya tatu baada ya kumshushia mpinzani wake makonde mfululizo yaliyompeleka sakafuni na kushindwa kuinuka hata alipohesabiwa.

Bondia huyo kutoka Ireland amecheza mapambano kumi ya ngumi za kulipwa na ameshinda yote na akifanikiwa kutetea atakuwa ameendeleza rekodi yake ya ushindi.

Awali pambano la Katie na Cindy lilipangwa kufanyika mjini Chicago Oktoba 6, lakini limehamishiwa Boston kwa kuwa siku hiyo litapigwa pambano jingine la ubingwa wa Dunia kati ya Billy Joe Saunders atakayetetea ubingwa wake wa WBO.

Katika pambano hilo la bingwa wa WBO, Saunders raia wa Uingereza atatetea taji lake kwa kuzichapa na Demetrius Andrade wa Marekani, uzani wa middle, kwenye ukumbi wa TD Garden.

Promora wa pambano hilo Eddie Hearn, alisema kuwa wameamua kuyaunganisha mapambano hayo ili kuwapa burudani mashabiki wote wa ngumi.