Bifu la Sneijder na Van Persie laibuka upya Uholanzi

Muktasari:

Wengi walidhani ugomvi wa wawili umekwisha, lakini kumbe mambo ndio kwanza yameanza. Jambo hili linafichua ugomvi wa wawili hao. Hivi karibuni, Wesley Sneijder alistaafu soka la kimataifa na alifanyiwa tukio maalumu la kumuaga.

WESLEY Sneijder dhidi ya Robin van Persie. Masupastaa hao wa Uholanzi ni maadui wakubwa licha ya kwamba waliwahi kucheza pamoja kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo.

Wengi walidhani ugomvi wa wawili umekwisha, lakini kumbe mambo ndio kwanza yameanza. Jambo hili linafichua ugomvi wa wawili hao. Hivi karibuni, Wesley Sneijder alistaafu soka la kimataifa na alifanyiwa tukio maalumu la kumuaga.

Lakini, mwenyewe amechagua kikosi chake cha mastaa aliowahi kucheza nao timu moja, ili acheze mechi ya mwisho ya kuagwa kwenye soka akafanye mambo yake mengine. Hapo ndipo utamu kamili ulipowadia.

Sneijder hakumjumuisha Van Persie kwenye kikosi chake cha kwanza. Kiungo huyo wa Kidadi, ameamua kuchagua washambuliaji watatu, Zlatan Ibrahimovic, Samuel Eto’o na Arjen Robben kuingia kwenye kikosi chake cha kwanza.

Kuhusu Ibrahimovic, Sneijder alisema kwamba alikuwa mtu safi sana kwake. Hapo ndipo lilipokuja swali la kama Ibra alikuwa mtu safi kwake, nani hakuwa mtu safi. Wanazengwe wakaenda moja kwa moja kumtaja yule aliyemfungia vioo kwenye kikosi chake, straika Van Persie. Kumbe ugomvi wao haujakwisha.

Ilielezwa kwamba ugomvi wa wawili hao ulianza kwenye tukio la nani apige mpira wa adhabu kwenye Euro 2008. Lakini, taarifa za ndani zimedai wawili hao walitibuana kabla ya tukio hilo.

Mambo yalianzia mazoezini, ambapo Van Persie alimchezea rafu Sneijder. Kilichoonekana ni kwamba Van Persie alikuwa akijaribu kumuumiza mwenzake makusudi mazoezini. Sneijder, hakupenda jambo hilo na aliamua kwenda kuliweka wazi kwenye vyombo vya habari itambulike. Hapo ikachochea zaidi malumbano.

Siku chache baadaye, wakatibuana tena kwenye mechi dhidi ya Russia, ambayo ilimalizika kwa Uholanzi kuchapwa 3-1. Wakiwa nyuma kwa bao 1-0, Uholanzi walipata faulo nje ya eneo la hatari. Sneijder ndiye aliyekuwa fundi wa kupiga mipira hiyo ya faulo, hivyo alitazamiwa yeye kupiga. Lakini, Van Persie akakimbilia mpira, akaenda kupiga na kukosa.

Mechi ikaisha. Miezi minne baadaye, Sneijder, alibaki na dukuduku na kuamua kuliweka bayana kwenye gazeti moja huko Uholanzi.

Alisema Van Persie amekiuka makubaliano na kuongeza: “Tangu mwanzo kabisa, nilichaguliwa kuwa mimi ndiye mtu wa kupiga faulo zote, hakuna mwingine anayepaswa kugusa mpira.”

Kusikia hivyo, Van Persie, alikwenda kuzungumza na gazeti jingine na kujibu mapigo, akisema: “Nilitarajia kitu cha maana zaidi kutoka kwa Wesley. Ni kitu cha ajabu kuzungumza kwamba ni yeye tu ndiye mwenye uwezo wa kupiga mipira ya faulo. Nendeni kamuulizeni kocha.”

Van Persie akadai kwamba hataki tena kuzungumza na Sneijder kumaliza jambo hilo baina yao kwa sababu kiungo huyo amezungumza hadharani. Fowadi huyo wa zamani wa Manchester United na Arsenal, Van Persie alisema labda kwenye suluhisho lao, basi nchi nzima uhusishwe, ije kwenye mkutano. Mwaka 2013, ikiwa imepita miaka mitano tangu walipotibuana, Sneijder alionekana kama amesahau yaliyopita, ambapo alimchagua Van Persie wakati huo akiwa Man United, kwenye tuzo ya Ballon d’Or. Lakini, kitendo cha sasa kuamua kumchagua straika Ibrahimovich imeonyesha wazi kwamba Sneijder hajamsamehe ile kwa moyo mmoja, Van Persie. Sneijder, ambaye kwa sasa anacheza soka lake huko Qatar katika klabu ya Al-Gharafa, aliwahi kupita kwenye klabu matata kabisa Ulaya, Ajax, Real Madrid , Inter Milan, Galatasaray na Nice.

Kikosi chake bora alichokichagua ni kama kifuatacho; Julio Cesar; Christian Chivu; Sergio Ramos; Javier Zanetti, Marcelo, Clarence Seedorf, Guti, Dejan Stankovic, Samuel Eto’o’, Arjen Robben na Zlatan Ibrahimovich.