Bellamy afunguka ishu ya Bale na Man United

Gareth Bale

Muktasari:

Bale kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mpango wa kurudi Ligi Kuu England huku Manchester United ikipewa nafasi kubwa ya kumnasa hasa katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

CARDIFF, WALES. STAA wa zamani wa Manchester City, Craig Bellamy amedai Manchester United haitamsajili Gareth Bale kwa sababu haitaweza kumudu kulipa mishahara ya supastaa huyo wa Real Madrid.

Bale kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mpango wa kurudi Ligi Kuu England huku Manchester United ikipewa nafasi kubwa ya kumnasa hasa katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Mwishoni mwa msimu uliopita, staa huyo wa kimataifa wa Wales alifichua anafikiria kuihama Real Madrid kauli aliyotoa baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool, ambapo alitokea benchi na kufunga mara mbili, Los Blancos iliposhinda 3-1.

Kauli hiyo iliwachochea na kuipa matumaini Man United kwamba wanaweza kumsajili staa huyo, lakini Bellamy alisema haoni kama mchezaji huyo raia mwenzake wa Wales atakwenda Old Trafford.

“Wapi atakwenda? Man United hawezi kulipa mishahara yake na hakuna atakayeweza. Kuna klabu moja tu inayoweza kulipa mishahara ya mchezaji huyo,” alisema Bellamy.

“Hiyo ndiyo dunia aliyopo kwa sasa. Mishahara anayolipwa itabidi ipungue kama anataka kwenda kwenye timu nyingine. Huo ndio ukweli. Hakuna klabu itakayokubali kutumia Pauni 80 milioni au Pauni 90 milioni. Juventus wao wamefanya hivyo kwa Cristiano Ronaldo kwa madhumuni tofauti, kufanya biashara. Lakini, ukimchukua Bale hutarajii kupata faida ya nje ya uwanja. Labda kufanyike uhamisho wa kubadilishana wachezaji, lakini kwa kiwango cha Bale si mchezaji wakufanyiwa jambo hilo.”

Bale amefunga mabao 88 katika mechi 189 Real Madrid katika michuano yote.