Barcelona yaongeza dau la Willian

Muktasari:

Uamuzi wa Barcelona kutangaza ofa hiyo umetokana na kitendo cha Chelsea kuipiga chini ofa ya kwanza ya Pauni 50 milioni iliyowasilishwa na klabu hiyo kwa ajili ya Willian.

Barcelona, Hispania. Klabu ya FC Barcelona imeongeza dau kufikia Pauni 60 milioni kwa ajili ya uhamisho wa kiungo Willian kutoka Chelsea, anayehitajia na kocha Ernesto Valverde.

Uamuzi wa Barcelona kutangaza ofa hiyo umetokana na kitendo cha Chelsea kuipiga chini ofa ya kwanza ya Pauni 50 milioni iliyowasilishwa na klabu hiyo kwa ajili ya Willian.

Mwakilishi wa Barcelona, Ernesto Valverde, amebainisha klabu hiyo kuongeza dau akisema anaamini Chelsea watalainika kwa dau hilo jipya.

Taarifa hizo zimefichuliwa na mtandao wa Sportsmail, ambao uliobainisha pia kuhusu Chelsea kuipiga chini ofa ya awali ya Pauni 50 za Barcelona.

Imeelezwa kuwa mabingwa hao wa La Liga awali walipanga kuongeza Pauni 5 milioni lakini wakaona isiwe tabu wafikishe Pauni 60 milioni ili kutoipa Chelsea mwanya wa kumbania winga huyo.

Willian aling’ara sana katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia akiichezea Brazil ambayo iling’olewa na Ubelgiji katika robo fainali na mchezaji huyo anahitajiwa kwenda kuziba pengo la Andres Iniesta aliyeamua kuihama Barca na Paulinho aliyeuzwa kwa mkopo kwenda Japan, hivyo anatakiwa kwedna kuunda safu ya kiungo na Mbrazil mwenzake Philippe Coutinho.