Barcelona wasiwasi kibao kwa Willian

Muktasari:

Barcelona imekiri kuziogopa pesa za Man United kuwa zinaweza kuifanyia vurugu kwenye mpango wake wa kumsajili Willian.

BARCELONA, HISPANIA. MWENYE pesa sio mwenzako na hicho ndicho kinachoifanya Barcelona kuiogopa Manchester United katika mbio za kumfukuzia winga wa Chelsea, Mbrazili Willian.

Barcelona imekiri kuziogopa pesa za Man United kuwa zinaweza kuifanyia vurugu kwenye mpango wake wa kumsajili Willian.

Ijumaa iliyopita, Barca ilipeleka ofa yake ya tatu huko Chelsea ikimtaka Willian kwa ada ya Pauni 55 milioni.

Lakini staa huyo wa Brazil anawindwa pia na Jose Mourinho wa Man United na hilo linaitisha Barcelona kwa sababu Man United ina pesa ya kutosha tu kulipa kumsajili Willian.

Willian mpango wake ni kuachana na Chelsea kwenye dirisha hili, lakini Barcelona licha ya kupeleka ofa yake bado haijapata mapokezi yoyote mazuri kutoka kwa wababe hao wa Stamford Bridge.

Taarifa zinadai Willian mwenyewe anashawishika kwenda Barcelona, lakini kama kutakuwa na mzigo mkubwa kutoka Man United, basi Chelsea inaweza kukaa mezani kufanya biashara hasa ikizingatiwa mpango wake ni kumchukua Anthony Martial kwenda kuziba pengo la Eden Hazard kama atakwenda zake Real Madrid.

Ripoti za kutoka Old Trafford zinadai Manchester United kwa sasa inapiga hesabu za kumsajili beki wa kati Harry Maguire na ipo tayari kutoa Pauni 65 milioni kupata saini yake. Mourinho anamwinda pia winga Ivan Perisic wa Inter Milan.