Barca yaitaka Arsenal kuacha ubaili

Muktasari:

Arsenal iliyosifika kwa ubahili wakati ikinolewa na Arsene Wenger, itachuana na mahasimu wao wa jiji la London, Tottenham Hotspur ambayo nayo inamuwania Andre Gomes.

Barcelona, Hispania. Klabu ya FC Barcelona imeweka wazi kuwa Arsenal inayo nafasi ya kumsajili kiungo chipukizi Andre Gomes mwenye miaka 23 iwapo watakuwa tayari kutoa Pauni 20 milioni.
Arsenal iliyosifika kwa ubahili wakati ikinolewa na Arsene Wenger, itachuana na mahasimu wao wa jiji la London, Tottenham Hotspur ambayo nayo inamuwania Andre Gomes.
“Barcelona itakua tayari kumuuza Andre Gomes kwa Pauni 20 milioni, kwa klabu yoyote inayomuhitaji,” ilisema taarifa ya klabu hiyo leo asubuhi.
Kiungo huyo mshambuliaji amefunga mabao matatu katika mechi 75 alizoichezea Barcelona tangu alipojiunga nayo kwa ada ya Euro 35 milioni mwaka 2016 akitokea Valencia.
Kocha mpya wa Arsenal, Unai Emery amekuwa na sera tofauti na Wenger, kwani tayari ameshawasajili chipukizi Matteo Guendouzi kutoka Lorient na mlinzi mkongwe wa Juventus na Uswisi, Stephan Lichtsteiner.
Wengine ambao Emery ameshawasajili ni mlinzi wa Borussia Dortmund, Sokratis Papastathopoulos, kipa wa Bayer Leverkusen, Bernd Leno na kiungo wa Sampdoria, Lucas Torreira.