Bale awafuta kabisa Arsenal kwenye rada zake

Muktasari:

Lakini, wakala wake anasema hivi, kama ataamua kuondoka, basi atakwenda kota hata mwezini, lakini si kwenda kujiunga na Arsenal.

MADRID, HISPANIA. GARETH Bale anajiandaa kufanya mazungumzo na mabosi wa Real Madrid kuhusu hatima yake, atabaki au ataondoka.

Lakini, wakala wake anasema hivi, kama ataamua kuondoka, basi atakwenda kota hata mwezini, lakini si kwenda kujiunga na Arsenal.

Nyie watu wa Washika Bunduki wa Emirates mpo? Staa huyo, ambaye amefunga mabao mawili kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool na kuwasaidia Real Madrid kubeba taji lao la tatu mfululizo kwenye michuano hiyo.

Kwenye mechi hiyo, Bale alianzia benchi na hilo ndilo linalomtatiza na kutaka kuachana na timu hiyo kwenda kwingineko, ambako atakuwa na wakati mzuri wa kupata nafasi ya kuanza katika kila mechi.

Bale anataka kubaki Real Madrid, lakini kwanza ahakikishiwe nafasi ya kuanza kwenye kikosi hicho cha Bernabeu, kama itakuwa vinginevyo basi atafungua mlango wa kutokea, lakini kwa mashabiki wa Arsenal wasahau kupata huduma yake, wataishia kumwona tu kwa wapinzani wao.

Akizungumza juu ya hilo, wakala wa staa huyo wa kimataifa wa Wales, alisema Bale hivi karibuni atafanya mazungumzo na mabosi wa Madrid kutambua hali ya mambo ilivyo na hatima yake kwenye kikosi.

Mwenyekiti wa Stellar Group, Jonathan Barnett alisema: “Nadhani tutakuwa na mazungumza na Real Madrid na kuona tunakwendaje. Anataka nafasi na kuwa na mwaka mzuri kuliko mwaka uliopita. Anataka kucheza zaidi, hilo ndilo kubwa lililopo kwenye akili yake.

“Nadhani yeye ni mmoja kati ya wachezaji watatu au wanne waliobora kabisa katika sayari hii ya dunia. Kwa mtu wa aina yake, anapaswa kupata nafasi ya kucheza na siyo suala la pesa.

“Anataka kushinda Ballon d’Or na nadhani anaweza. Nadhani ni Mwingereza bora kabisa kwa wachezaji wanaocheza ng’ambo na hilo halina mjadala, kwa sababu sota tunafahamu uwezo wake.

“Nadhani mabao yake kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yanaeleza kila kitu. Anafahamika kwa ubora wake na sote tunafahamu hilo, japo mwenyewe anafahamu hajaonyesha ule ubora wake halisi.”

Real Madrid wanahitaji ada inayokaribia Pauni 200 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo, lakini kama kutaletwa ofa ya Pauni 180 milioni basi biashara itafanyika.

Bale hakutaka kuruhusu mshahara wake ushuke kwenda kujiunga na timu nyingine, hivyo aliendelea kubaki Real Madrid hata kama alikuwa hana uhusiano mzuri na kocha Zinedine Zidane huko Bernabeu. Lakini, kwa sasa Zidane ameondoka na timu hiyo ipo chini ya kocha mpya.

Staa huyo aliondoka Tottenham kwenda kujiunga na Real Madrid mwaka 2013 kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwenye uhamisho kwa wakati huo, Pauni 86 milioni. Miaka miwili iliyopita, Bale alisaini mkataba mpya unaomshuhudia akilipwa Pauni 650,000 kwa wiki kabla ya makato ya kodi na mkataba ho utafika tamati 2022.

Wakala wa Bale, Barnett, ambaye ni shabiki wa Arsenal, amekiri kwamba hakuna uwezekano wowote wa mchezaji huyo kwenda kujiunga na timu hiyo yenye maskani yake huko Emirates.

“Ningependa sana kumwona akicheza Arsenal, lakini ninachokiona ni rahisi kwenda mwezini kuliko hilo kutokea. Anayapenda maisha yake ya Hispania, ana watoto watatu, lakini subiri tuone kwa sababu ni lazima acheze soka,” alisema.

Staa huyo amekuwa akihusishwa na Man United kwa siku za karibuni na kama dili la Madrid likikwama basi anaweza kuibukia Old Trafford.