Arturo Vidal analeta balaa

Muktasari:

Chelsea na Manchester United zimeripotiwa kupigana vikumbo katika kuiwania huduma ya kiungo huyo mwenye mapafu ya umbwa anapokuwa uwanjani.

MUNICH, UJERUMANI. GHAFLA tu Arturo Vidal anatarajia kuanzisha vita kali kwa vigogo wa Ligi Kuu England baada ya kudaiwa Bayern Munich ipo tayari kumpiga bei supastaa huyo wa kimataifa wa Chile.

Chelsea na Manchester United zimeripotiwa kupigana vikumbo katika kuiwania huduma ya kiungo huyo mwenye mapafu ya umbwa anapokuwa uwanjani.

Kwa muda mrefu Vidal amekuwa akiwindwa na timu hizo mbili tangu alipokuwa Juventus kabla ya kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Ujerumani na kubeba ubingwa mara kadhaa kwenye Bundesliga.

Staa huyo atarejea uwanjani akitokea kuuguza majeraha yake ya upasuaji wa goti na huenda akaenda kujiunga na moja ya timu hizo mbili, wakati huu akiwa na umri wa miaka 31. Bayern Munich ipo chini ya kocha mpya, Niko Kovac na mpango wake ni kupitisha fagio kwenye kikosi hicho, akidai atakuwa tayari kupokea kiasi cha Pauni 31 milioni katika kumuuza nyota huyo. Kiwango hicho cha pesa kinaweza kumshawishi kocha mpya wa Chelsea, Maurizio Sarri akaamua kumsajili baada ya kudai timu yake haina wachezaji wengi wenye viwango wakati alipotambulishwa huko Stamford Bridge.

Kocha Jose Mourinho anahitaji kiungo pia kwenye kikosi chake cha Man United na anaamini Vidal ni staa wa kiwango hicho.