Arsenal yampandia dau Mesut Ozil

Muktasari:

Kocha wa Manchester United Jose Mourinho anamtaja Ozil ni mmoja wa wachezaji bora wa kiungo duniani

London, England. Kocha Arsene Wenger bado anaweweseka na kiungo wake Mesut Ozil, baada ya kumtangazia dau kubwa la mshahara katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Arsenal imepanga kumpa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mshahara wa zaidi ya Pauni 235,000 kwa wiki ili kumbakiza Emirates.

Taarifa hizo ni mpya kwa Arsenal ambayo awali ilidai itampiga bei Ozil katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani kabla ya kusogeza mbele hadi majira ya kiangazi.

Klabu za Manchester United na Barcelona zinafuatilia kwa karibu usajili wa Ozil na kila moja imepanga kumpandia dau kumsajili baada ya mkataba wake kumalizika majira ya kiangazi.

Mjerumani huyo aligoma kutia saini mkataba mpya akidai mkataba wake uboreshwe kwa kulipwa mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki.

Mbali na Ozil, mshambuliaji Alexis Sanchez aligoma kutia saini mkataba mpya akidai mshahara mnono. Nyota hao wamekuwa wakimpasua kichwa kocha huyo muda mrefu.

Baada ya kutupiwa lawama akidaiwa kucheza chini ya kiwango, Ozil amerejesha makali yake katika mechi za hivi karibuni akicheza kwa kiwango bora michezo ya Ligi Kuu England.

Klabu hiyo ina matumaini mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid, anaweza kumwaga wino baada ya kumpandia dau la mshahara ili kubaki Emirates.

Endapo Ozil atakubali kutia saini mkataba mpya, atakuwa ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mnono zaidi katika historia ya klabu hiyo kongwe nchini humo.

Arsenal haitaki kuwapoteza wachezaji hao ambao ni lulu katika medani ya soka Ulaya kutokana na ubora wao. Sanchez alitua Arsenal kutoka Barcelona.