Aguero azimia Argentina ikipokea kipigo

Muktasari:

Aguero alizimia ndani ya vyumba vya kuvalia nguo wakati wa mapumziko katika mchezo ambao Argentina ikiwa nyumbani ilishinda mabao 4-2.

Russia. Mshambuliaji Sergio ‘Kun’ Aguero, amezimia katika mchezo baina ya Argentina na Nigeria uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Krasnodar, Russia.
Aguero alizimia ndani ya vyumba vya kuvalia nguo wakati wa mapumziko katika mchezo ambao Argentina ikiwa nyumbani ilishinda mabao 4-2.
Mchezaji huyo wa Manchester City  hakuendelea na mchezo huo na baadaye aliwahishwa hospitali kwa uchunguzi.
Hata hivyo, Aguero mwenye miaka 29, aliruhusiwa baada ya madaktari kubaini ana afya njema na anaweza kuendelea na majukumu mengine.
Kocha wa Man City Pep Guardiola anasubiri taarifa ya madaktari kuhusu afya ya mpachika mabao huyo.
Mshambuliaji huyo mwenye kiwango bora cha kufunga mabao, alirejea uwanjani hivi karibuni akitokea katika maumivu kabla ya jana kuzimia.
Chama cha Soka Argentina kilitoa taarifa ya mchezaji huyo kuzimia na kuwahishwa hospitali kwa uchunguzi wa afya kabla ya kuruhusiwa.
Pia kocha wa Argentina Jorge Sampaoli alisema mchezaji huyo alizimia wakati mapumziko na hakurejea uwanjani kuendelea na mchezo.
Man City ilitoa taarifa ya mchezaji huyo alitakiwa kurejea haraka England kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Leicester City utakaochezwa wikiendi hii.
“Sergio alipata tatizo la kupumua, lakini aliwahishwa hospitali kwa uchunguzi wa awali. Madaktari wa klabu watamchunguza zaidi kwa tuna safari ya kuifuata Leicester City,” ilisema taarifa ya Man City.
Daktari wa Argentina Donato Villani alisema Aguero aliwahi kubainika na tatizo la moyo akiwa na miaka 15, lakini alipata matibabu na yuko fiti kwa asilimia 100.