Wamebakiza saa tu

HII inaitwa pambana na hali yako. Makocha wa Ligi Kuu England hasa wale wa Top Six kila mmoja kijasho kinamtoka akitafuta namna nzuri ya kufunga dirisha la usajili wa wachezaji litakalofungwa leo Alhamisi.

Kuna makocha hao wanakimbizana na muda. Jose Mourinho, Jurgen Klopp, Maurizio Sarri, Pep Guardiola, Mauricio Pochettino na hata Unai Emery kila mmoja anahitaji walau kufanya usajili wa mwisho kabla ya dirisha kufungwa.

Shughuli anayo Mourinho huko Manchester United, ambapo anahitaji saini ya zaidi ya mchezaji mmoja ili kuwa na uhakika wa kufanya vyema kwenye msimu huu ambapo Ligi Kuu England kwa upande wao itaanza kesho Ijumaa kwa mechi kali dhidi ya Leicester City huko Old Trafford.

Mourinho kichwa kinampasuka akitaka huduma za beki wa kati na winga mmoja matata. Lakini, mambo yatakuwa magumu zaidi kwa upande wake kama Paul Pogba, ataondoka baada ya Barcelona kuonekana kupania kuhitaji saini yake.

Kwenye kuziba pengo la Pogba kama ataondoka, Mourinho atamhitaji Sergej Milinkovic-Savic, lakini mabeki wa kati anaowataka ni Harry Maguire, Yerry Mina, Jerome Boateng na Toby Alderweireld.

Katika winga, Man United imeripotiwa inaweza kumsajili staa wa Chelsea, Willian kabla ya dirisha hilo kufungwa. Kumbuka dirisha linafungwa leo.

Kocha Emery huko Arsenal, ameripotiwa yupo kwenye hatua za kumnasa Ousmane Dembele kutoka Barcelona. Klopp anaweza kutimiza ndoto zake za kumnasa Nabil Fekir, baada ya kocha anayemnoa staa huyo huko Lyon, Bruno Genesio amefichua mchezaji huyo anataka kuhama na Liverpool inaweza kufanya maajabu yake kwa kumdaka katika dakika za mwisho kabisa. Staa mwingine ambaye ametajwa anaweza kunaswa kwenye dirisha hili ni Mateo Kovacic wa Real Madrid, ambaye anaweza kunaswa na Kocha Sarri huko Chelsea kabla ya dirisha halijafungwa.

Kiungo huyo wa kati amekuwa akihusishwa pia na Liverpool ya Klopp na Man United ya Mourinho. Guardiola ni kama amefunga duka vile, lakini endapo kutatokea usajili wowote atakaofanya kabla ya dirisha kufungwa, basi utahusisha kiungo wa kati baada ya kuwakosa Jorgino na Fred. Hiyo orodha ya wachezaji waliotajwa hapo ndiyo wanaoweza kuhama kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa kwenye Ligi Kuu England leo.