Madrid yatangaza hali ya hatari mrithi wa Ronaldo

REAL Madrid imetangaza hali ya hatari kwa klabu mbili wakati huu ikitarajia kununua mchezaji mwenye jina kubwa kwa ajili ya kurithi nafasi ya Cristiano Ronaldo aliyeondoka Santiago Bernabeu juzi Jumatano mchana.

Kwanza Madrid inaweza kumchukua yoyote kati ya Neymar au Kylian Mbappe kutoka PSG, lakini pia mabosi wa timu hiyo wameelekeza macho yao kwa staa wa Chelsea, Eden Hazard ambaye ameng’ara katika Fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ubelgiji.

Ronaldo ameacha pengo kubwa baada ya kutimkia Juventus kwa dau la Pauni 88 milioni na Real Madrid inatazamia kutumia dau hilo na nyongeza juu kwa ajili ya kumpata staa mmoja mwenye jina kubwa kuziba pengo lake.