Mwisho wa Zama

NI mwisho wa zama. Sasa ni wazi staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo anatarajiwa kufungua ukurasa mwingine wa maisha yake ya soka kwa kujiunga na Juventus kwa dau la Pauni 88 milioni katika dirisha hili la uhamisho.

Ilianza kama uvumi wa kawaida lakini watu wawili muhimu katika soka, mmoja kutoka upande wa Hispania na mwingine kutoka upande wa Italia wamethibitisha Ronaldo anakaribia kufungua historia nyingine ya maisha yake ya soka.

Alhamisi usiku mazungumzo baina ya wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes na Rais wa Real Madrid yalifanyika na mchambuzi mahiri wa soka la Hispania, Guillem Balague alikiri Ronaldo amewaambia Madrid anataka kuondoka.

“NI wazi kabisa Real Madrid na Cristiano Ronaldo kila mmoja anajua dhumuni la mwenzake. Kulikuwa na kikao kati ya wawakilishi wa Ronaldo na Real Madrid juzi usiku na Ronaldo aliweka wazi anataka kuondoka. Hicho ni kitu pekee ambacho anataka kufanya,” alisema Balague ambaye anaheshimika kwa habari za uhakika.

“Hatimaye Real Madrid imekubali na kusema ‘sawa kama mtu akija na Euro 100 milioni basi tutakuruhusu uondoke’. Hapo ndipo mambo yaliposimamia. Juventus imemwambia Mendes na Ronaldo watatao ofa hiyo na yeye mwenyewe watamlipa Pauni 26 milioni kwa mwaka na watafurahia kumpatia mkataba wa miaka minne.”

“Hicho ndicho ambacho Ronaldo anataka. Hiki ni kitu kipya kwa mara ya kwanza kutokea katika madirisha makubwa matatu ya uhamisho yaliyopita. Real Madrid ipo tayari kabisa jambo hili litokee,” alisema Balague.

Kwa upande wa Italia ambako Ronaldo anatazamiwa kucheza ligi kubwa ya tatu barani Ulaya, Rais wa zamani wa Juventus, Luciano Moggi amedai dili la Ronaldo kwenda Juventus limeshakamilika kwa mujibu wa watu wake wa karibu na mchezaji huyo

“Kwa mtazamo wangu, tayari amesaini na amefaulu vipimo vya afya vya Juventus akiwa Munich. Hiki ndicho kitu ambacho ninafikiria baada ya kuzungumza na watu wangu muhimu,” alisema Moggi ambaye alikuwa bosi wa Juventus kwa miaka 12 kabla ya kukumbukwa na kashfa ya upangaji wa matokeo mwaka 2006 ambayo iliishusha daraja klabu hiyo.

Mtu mwingine aliyetia chumvi katika uhamisho wa Ronaldo kwenda Juventus ni wakala wake, Jorge Mendes ambaye akizungumza na gazeti moja la kwao Ureno alidokeza kuhusu dili hilo akidai itakuwa changamoto mpya kwa mteja wake.

“Kama hilo likitokea itakuwa hatua mpya, changamoto mpya katika maisha yake mazuri ya soka. Kama Ronaldo akiondoka Real Madrid atakuwa ana shukrani kubwa kwa klabu, rais, wakurugenzi, timu ya madaktari, na wafanyakazi wote pia na mashabiki wote wa Real Madrid duniani,” alisema Mendes.

Ronaldo alinunuliwa na Real Madrid akitokea Manchester United kwa dau la Pauni 80 milioni ambalo lilivunja rekodi ya uhamisho ya dunia wakati huo. Kuanzia hapo ametamba katika soka kando ya hasimu wake mkubwa Lionel Messi ambapo kila mmoja ametwaa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mara tano.

Tangu Desemba mwaka jana staa huyo ameingia katika malumbano na mabosi wa timu yake akiamini hawamtendei haki kwa kutomuongezea mshahara kama walivyohafikiana na kwa sasa anadai Madrid haimthamini tena.