Ozil macho kodo kwenye jezi Namba 10 Arsenal

ADIDAS inaripotiwa kuwa nyuma ya mpango wa kiungo Mesut Ozil kulazimisha kupewa jezi yenye namba 10 mgongoni kwenye kikosi cha Arsenal baada ya Jack Wilshere kuachwa.

Wilshere anaachana na Arsenal kwenye dirisha hili la uhamisho baada ya mkataba wake kufika ukingoni na sasa anaacha jezi yenye namba 10 bila mwenyewe jambo linalomfanya Ozil achangamkie kuipata kabla ya msimu mpya kuanza.

Kiungo huyo Mjerumani anataka jezi Namba 10 aivae msimu ujao kwa dhamira kubwa ya matangazo ya kibiashara.

Ozil alisaini dili safi la viatu na adidas, lakini wadhamini hao wanaamini kwamba jezi namba 10 inauzika zaidi sokoni hivyo wanamtaka mteja wao huyo awe na namba hiyo kwenye jezi yake.

Kwenye timu ya taifa ya Ujerumani, Ozil ameshakabidhiwa jezi huyo hivyo kilichobaki ni Arsenal tu kumpa na kumfanya staa hiyo kuweka sawa nembo yake kwenye masuala ya biashara.