Jina la Lukaku latua Madrid

IWAPO kweli lisemwalo lipo, basi ndiyo kama ulivyosikia kwamba Real Madrid imeanza kumtolea macho straika, Romelu Lukaku na inataka kumsajili kabla mwaka huu haujaisha.

Straika huyo wa Manchester United kwa sasa anafurahia wakati mzuri kabisa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia akiwa na kikosi cha Ubelgiji ambapo amefunga mara nne, akipiga mbili katika kila mechi kuisaidia nchi yake kutinga hatua ya 16 Bora.

Lukaku alitupia mbili dhidi ya Panama, kisha akafanya hivyo tena dhidi ya Tunisia na hivyo kulingana na Cristiano Ronaldo kwa mabao. Kwa kuona makali hayo, Real Madrid, sasa wanapiga hesabu za kumsajili ili akaongeze nguvu kwenye kikosi hicho.

Habari zinasema mabingwa hao wa Ulaya wanamtazama Mbelgiji huyo kuwa ni mtu mwafaka wa kwenda kuchukua nafasi ya Karim Benzema, ambaye sasa umri unazidi kumtupa mkono na klabu hiyo inaanza kuona kama hakuna kitu chenye manufaa zaidi watakivuna kutoka kwa mchezaji huyo.

Na sasa wanachoamini ni kwamba watakuwa wameongeza mabao mengi zaidi katika kikosi chao kama watafanikiwa kumnasa Lukaku, mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na Everton.

Kocha wa Man United, Jose Mourinho, alitibuana na Lukaku baada ya kudai kwamba alijifanya mgonjwa akae nje kwenye mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea ili kujiweka fiti kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia za huko Russia.