Liverpool yaweka mzigo kwa Asensio

LIVERPOOL imeripotiwa kuweka mezani kitita cha Pauni 150 milioni kwa ajili ya kumsajili staa wa Real Madrid, Marco Asensio.

Kiungo huyo wa Kihispaniola anatajwa kuwa mmoja wa makinda wenye vipaji vikubwa vya soka waliopo Ulaya kwa sasa baada ya kuibukia kwa kasi katika kikosi cha Los Blancos.

Liverpool inaripotiwa imeshaweka mkwanja wake mezani ambao utatosha kabisa kuwashawishi Madrid kuvunja mkataba wa mchezaji huyo huko Bernabeu.

Wanachokiamini wakali hao wa Anfield wanaonolewa na Mjerumani Jurgen Klopp ni kwamba Asensio atakwenda kuongeza ufundi kwenye kikosi chao atakapocheza nyuma ya washambuliaji watatu; Roberto Firmino, Mo Salah na Sadio Mane.

Mkataba wa Asensio huko Real Madrid utafika tamati Juni 2023 na imeripotiwa kwamba mkataba wake una kipengele cha kuhitaji kulipwa Pauni 615 milioni ili uvunjwe.

Kama dili hilo litakubalika basi Asensio atakuwa mchezaji ghali namba tatu duniani nyuma ya wakali wawili wa PSG, Neymar na Kylian Mbappe.