Chelsea kumtumia Costa ishu ya Conte

CHELSEA kwa sasa inahangaika kupata namna nzuri ya kumfuta kazi kocha Antonio Cointe na kisha imlipe fidia kidogo na imepata ujanja wa kumtumia Diego Costa katika kutimiza mpango huo.

Chelsea bado inashindwa kutangaza kocha mpya ikiwa zimebaki wiki sita tu kabla ya msimu mpya kuanza na jambo hilo linakuwa gumu kwa sababu Conte ameendelea kusisitiza anataka kumalizia mwaka wake mmoja uliobaki Stamford Bridge.

Conte anafanya hivyo ili alipwe fidia ya Pauni 9 milioni, lakini sasa Chelsea inataka kupunguza fidia hiyo kwa kumbana kocha huyo Mtaliano kwamba aliwaharibia biashara wakati wanamuuza Diego Costa kwenda Atletico Madrid.

Chelsea inadai kwamba walilazimika kumuuza Costa kwa Pauni 59 milioni kwenye dirisha la Januari kwa sababu Conte alimtumia meseji mchezaji huyo kwamba amefukuzwa kikosini, hapo iliwapa urahisi Atletico kulipa pesa kidogo la sivyo hakuna timu nyingine ambayo ingekuja kumchukua kwa ofa kama waliotoa wao.

The Blues inaamini Costa angeuzwa kwa pesa nyingi kama Conte asingefanya ambacho amekifanya na kutokana na hilo inataka kutumia hasara hiyo kwenye fidia ya kocha huyo ili wasimlipe Pauni 9 milioni zote anazohitaji.