Shabiki wa Man United anataka kuinunua Chelsea

BILIONEA Roman Abramovich amelazimika kutumia nguvu kugomea ofa matata kabisa kutoka kwa tajiri wa Kiingereza, Jim Ratcliffe, aliyetaka kuinunua Chelsea.

Ripoti zinadai Ratcliffe, ambaye ni shabiki wa Manchester United anatajwa kuwa na utajiri wa Pauni 20 milioni, ikiwa na maana ana pesa nyingi kuliko bilionea huyo wa Stamford Bridge, ambaye kwa sasa anashindwa kuingia Uingereza kwa kukosa kibali.

Roman kwa sasa amepigwa marufuku kuingia Uingereza jambo linalokwamisha mambo mengi ikiwamo mpango wa kuupanua Uwanja wa Stamford Bridge na kutokana na hilo, tajiri mwingine akaamua kuja kutaka kuinunua Chelsea kitu ambacho Mrusi huyo amegoma na kudai hawezi kuiuza timu yake hata kama hataruhusiwa kuingia kwenye nchi hiyo.

Abramovich aliinunua Chelsea kwa Pauni 140 milioni mwaka 2003 na ripoti za karibuni zilidai bilionea huyo anaweza kupokea ofa ya Pauni 2 bilioni kama kutakuwa na tajiri atakayetaja kuibeba The Blues.

Hata hivyo, bilionea huyo shabiki wa Man United si yeye tu aliyetaka kuinunua Chelsea, mabosi wengine ni wa kutoka China, lakini Abramovich wote aliwakatalia. Ratcliffe ni shabiki wa Man United, lakini ana tiketi za msimu huko Stamford Bridge.

“Kutoa Pauni 2 bilioni au pesa inayozidi hapo kidogo ni kama tone la maji baharini kwa Jim,” alisema mmoja wa marafiki wa karibu wa bilionea huyo.