Kumbe Conte kakataa ofa ya kuinoa Madrid

KOCHA Antonio Conte ameripotiwa kukataa nafasi ya kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Real Madrid ya Hispania.

Kocha huyo Mtaliano anatarajia kuondoka Stamford Bridge kwenye majira haya ya kiangazi baada ya kuripotiwa kutibuana mara kadhaa na bodi na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.

Lakini, jambo hilo halikumfanya akubali ofa ya kwenda kuvaa viatu vya Zinedine Zidane, ambaye ameamua kujiuzulu Real Madrid muda mfupi tu baada ya kuwapa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa tatu mfululizo.

Mwandishi mmoja wa habari Mtaliano, Gianluca Di Marzio, alisema Madrid walifanya mawasiliano na Conte, lakini kocha huyo aligoma suala la kwenda kuwa kocha wa timu hiyo.

Conte, ambaye aliwahi kuinoa Juventus, alishinda ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wake wa kwanza tu huko Chelsea na msimu uliomalizika hivi karibuni alibeba ubingwa wa Kombe la FA akiwachapa Manchester United kwenye fainali.

Kama ataondoka Chelsea basi atalipwa fidia ya Pauni 9 milioni na Conte hataki kuipoteza fursa hiyo, hivyo hawezi kukubali ofa kutoka kwa klabu nyingine anasubiri kwanza hadi Chelsea wenyewe wamfukuze.

Madrid kwa sasa wanatafuta kocha mpya na wengi wametajwa akiwamo Jurgen Klopp wa Liverpool na Massimiliano Allegri wa Juventus, huku kukiwa na ripoti Guti anaweza kupewa dili hilo.