£307m Mkwanja wa kumvuta Neymar Bernabeu

KWANI kuna habari gani! Neymar Pauni 300 milioni? Hii sasa kufuru.

Real Madrid wamepanga kumfanya Neymar kuvunja rekodi nyingine kwenye uhamisho baada ya kupanga kumng’oa kutoka Paris Saint-Germain kwa ada ya Pauni 307 milioni. Pesa hiyo imezidi kiwango cha pesa ambacho wababe hao wa Ufaransa wameripotiwa kukiweka kama kipengele kwenye mkataba wa mchezaji huyo kwamba kiasi hicho kikilipwa, basi biashara inafanyika.

Chanzo cha karibu na Real Madrid kililiambia SunSport PSG waliweka kipengele kwenye mkataba wa Neymar kinachosema kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kulipa Euro 300 milioni (Pauni 263 milioni) Septemba 1, mwaka jana siku moja baada ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka huo basi itamchukua mchezaji huyo.

Dili hilo lilifichua Neymar asingeweza kuichezea timu nyingine hadi itakapofika 2019. Kipengele hicho kiliwekwa kwa mpango maalumu hakutakuwa na timu itakayoweza kulipa pesa hiyo hivyo Neymar atakuwa kwenye kikosi hicho cha Parc des Princes walau kwa miezi 18 tangu pale ilipomsajili kwa Euro 224 milioni (Pauni 198 milioni) kwa wakati ule akitokea Barcelona. Ada hiyo iliweka rekodi ya dunia kwenye uhamisho mwaka jana.

Hata hivyo, Real Madrid hawataki kusubiri hadi Januari mwakani baada ya kuwa na mpango wa kuunda kikosi cha kibabe kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Kwa maana hiyo, kama uhamisho huo utafanyika utakuwa umevunja rekodi ya uhamisho iliyokuwa imewekwa na mchezaji huyo kwa Pauni 109 milioni zaidi.

Dili hilo pia litahamia kwenye masuala ya kibiashara na itashuhudia Nike, inayomdhamini Neymar ikiporwa mchezaji huyo na Adidas, ambao ndiyo wadhamini wa Real Madrid.

Ishu kubwa iliyopo, Real Madrid wataweza kulipa mishahara ya Neymar, ambayo ni kama Pauni 39 milioni, wakati huo huo wakiwa na mchezaji Cristiano Ronaldo kwenye kikosi chao, ambaye hawezi kukubali kufunikwa kwenye mshahara. Hilo ndilo linalofanya kwa sasa Madrid kuanza kumchunia Ronaldo na huenda akatafuta timu ya kwenda kwenye dirisha hili kumpisha staa wa Kibrazili kuja kuweka himaya yake. Ronaldo anaripotiwa kulipwa mshahara wa Pauni 18 milioni kwa mwaka hivyo kuwa na mishahara mikubwa ya aina hiyo itakuwa mzigo mkubwa kwa timu kitu ambacho Florentino Perez hataweza kukimudu.

Baada ya Kocha Zinedine Zidane kung’atuka klabuni hapo mwezi uliopita, ishu nzima sasa ya kusimamia dili la kumleta Neymar huko Bernabeu inasimamiwa na Perez na anaweza kufanikiwa kumnasa, lakini mfuko lazima utalazimika kumtoboka zaidi.