Kocha Klopp amshauri Ramos akacheze mieleka

Muktasari:

Chozi la Salah liko katika pande mbili, kuikosa fainali ya Ulaya na kushindwa kufanya kile alichokuwa anakiwaza lakini kikubwa ni kuzikosa Fainali za Kombe la Dunia

KILA kona ya dunia, kabla ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kati ya Real Madrid na Liverpool mashabiki wa soka walikuwa wanataka kuona mpambano wa Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah.
Kila mmoja alikuwa akisema yake, ukali wa mchezaji lakini hali ilikuwa tofauti, kabla ya hata mchuano haujakolea vizuri, beki wa Real Madrid, Sergio Ramos akakatisha matamanio ya watu.
Alitumia dakika 30 kufuta kilichokuwa kikifikiriwa na wengi. Alimuumiza Salah, lakini akajaribu kuendelea na mchezo ikashindikana akatoka huku akimwaga machozi.
Chozi la Salah liko katika pande mbili, kuikosa fainali ya Ulaya na kushindwa kufanya kile alichokuwa anakiwaza lakini kikubwa ni kuzikosa Fainali za Kombe la Dunia.
Hali hiyo imemfanya Ramos kupingwa kila kona hasa mashabiki wa Liverpool kwa kitendo chake cha kumchezea rafu mbaya na wakati Salah alipokuwa anatolewa nje, alikuwa akicheka tu.

Nyota huyo wa Misri alilazimika kutoka dakika ya 31 baada ya kuumizwa na Ramos kwani aliukamata mkono wa Salah na kumsababisha aanguke vibaya kiasi cha kufiukia bega.
Salah alikuwa akilia wakati anatolewa akiwaza ndoto yake kucheza Kombe la Dunia haipo tena. Wakati hali ikiwa hivyo, televisheni zilimnasa Ramos alikuwa akicheka na kutabasamu akiwa na mwamuzi msaidizi akiw apembeni ya uwanja.
“Ramos ni beki mzuri lakini kile alichokifanya si cha kiuanamichezo,” alisema mchezaji wa zamani, Gary Lineker wakati akiangalia televisheni ya BT Sport.
Wakati hali ikiwa hivyo, Ramos alituma salamu kwa Mohamed Salah akimpa pole lakini alisema kuwa haikuwa nia yake kumuumiza winga huyo wa Liverpool.
Kuumia kwa Salah ni baada ya beki huyo kumvuta mkono walipokuwa wakiwania mpira na kuanguka Ramos.
Bosi wa Liverpool, Jurgen Klopp alifananisha kitendo cha Ramos hadi kumuumiza mchezaji wake ni sawa na mieleka.
“Najua, anaposema hayo, lakini kikubwa ni kuumia kwa Salah na kitendo kama kile ni sawa na mchezo wa mieleka na bahati mbaya ameangukia bega."