Madrid yamtega Mo Salah

Muktasari:

Rais wa zamani wa miamba hiyo ya Bernabeu, Ramon Calderon, alisema kwa mchezaji mwenye kiwango bora kama cha Mo Salah, suala la kuhama timu ataliamua mwenyewe kwa sababu timu yake haiwezi kukubali kumuuza kirahisi rahisi tu.

UNAAMBIWA hivi, Real Madrid imeshaanza kumchokonoa Mohamed Salah kwa kutoa kauli kuwa hatima yake ya kujiunga na timu hiyo ipo mikononi mwake mwenyewe.

Rais wa zamani wa miamba hiyo ya Bernabeu, Ramon Calderon, alisema kwa mchezaji mwenye kiwango bora kama cha Mo Salah, suala la kuhama timu ataliamua mwenyewe kwa sababu timu yake haiwezi kukubali kumuuza kirahisi rahisi tu.

Calderon, ndiye aliyemnunua Cristiano Ronaldo kutoka Manchester United na mchezaji huyo alisubiri kwa mwaka mmoja kabla ya kutua Real Madrid, alipoamua mwenyewe kwa sababu wachezaji wa kiwango cha juu kuhama wanaamua wenyewe na ndiyo maana hilo litamhusu pia Mo Salah.

Ronaldo alisubiri mwaka mmoja kabla hajahamia Madrid. Philippe Coutinho naye alisubiri kwa muda kabla ya kuihama Liverpool kwenda kujiunga na Barcelona.

Calderon alisema: “Salah ni mchezaji mahiri. Nimekuwa nikimwona akifunga sana mabao kutoka kila eneo kwa sababu siku zote amekuwa kwenye nafasi mwafaka kwa wakati mwafaka. Kila timu ingehitaji kuwa na huduma yake, lakini ana mkataba na nina hakika Liverpool haiwezi kufurahia kuona anaondoka.

“Kwa jambo hilo, hapo wa kuamia ni mchezaji mwenyewe. Ukiwa mchezaji wa kiwango cha juu, uamuzi unakuwa juu yako.”

Liverpool ilimpo teza pia Luis Suarez, aliyetimkia Barcelona na sasa presha imekuwa kubwa kumpoteza Mo Salah, kwa sababu haiamini kama anaweza kuwa mtiifu kama Steven Gerrard, aliyeamua kubaki Anfield katika nyakati zote za ubora wake.

Madrid inamtaka Mo Salah na Calderon ameipa ujanja juu ya kumnasa staa huyo ni kumsubiri tu.

“Nilikumbana na hilo kwa Ronaldo na Man United, lakini mwingine tulifikia makubaliano. Aliahidi na kila kitu kilitimia,” alisema.