He! Henry kamtosa kiaina Mikel Arteta

Muktasari:

Ripoti zinadai Mfaransa huyo ambaye kwa miaka miwili ya karibuni amekuwa akifanya kazi chini ya Kocha Roberto Martinez kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Ubelgiji, amesema yupo tayari kurudi kuitumikia timu yake ya zamani kama atahitajika kufanya hivy

HABARI ndiyo hivyo. Thierry Henry amesema hivi anataka sana kurudi Arsenal, lakini si kwenda kufanya kazi na kocha anayetajwatajwa, Mikel Arteta.

Ripoti zinadai Mfaransa huyo ambaye kwa miaka miwili ya karibuni amekuwa akifanya kazi chini ya Kocha Roberto Martinez kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Ubelgiji, amesema yupo tayari kurudi kuitumikia timu yake ya zamani kama atahitajika kufanya hivyo.

Arsenal kwa sasa inaonekana kukaribia kumtangaza Kocha Msaidizi wa Manchester City, Arteta, licha ya kwamba Mhispaniola huyo kutokuwa na uzoefu wowote wa kuwa kocha mkuu katika kikosi kinachoshiriki mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Henry ameripotiwa wiki hii atakuwa na mazungumzo na Bodi ya Arsenal na kwenye mkutano huo atawasilisha mawazo yake.

Arsenal wenyewe wameripotiwa kufanya makubaliano ya mdomo juu ya kumpa Arteta dili la kuinoa timu hiyo iliyokuwa chini ya Arsene Wenger, aliyeng’atuka baada ya miaka 22.

Rekodi za Henry kwenye kikosi cha Arsenal enzi zake za uchezaji, alifunga mabao 228 katika mechi 376 alizoitumikia timu kwa nyakati mbili tofauti.

Arsenal imeripotiwa kuwachunia makocha wenye uzoefu kama Luis Enrique, Carlo Ancelotti, Massimiliano Allegri na Brendan Rodgers na kufikiria kumpa kazi Arteta, mtu ambaye Henry anaona bado hajakomaa kukabidhiwa majukumu hayo mazito.