Eti! Mourinho achoshwa na basi la Conte Chelsea

Muktasari:

United ililala bao 1-0 la penalti lililofungwa na staa wa kimataifa wa Ubelgiji, Eden Hazard huku Chelsea ikitwaa taji hilo kwa mara ya nane, lakini Mourinho anadai Manchester ilikuwa timu bora ingawa haikushinda.

ANTONIO Conte alimpiga Jose Mourinho juzi Jumamosi katika mbinu ambazo ni Mourinho mwenyewe amewafundisha makocha wengi wa zama hizi. Hata hivyo, Mourinho ameishia kuwalaumu Chelsea kwa kuchezesha wachezaji tisa wanaojihami tu.

United ililala bao 1-0 la penalti lililofungwa na staa wa kimataifa wa Ubelgiji, Eden Hazard huku Chelsea ikitwaa taji hilo kwa mara ya nane, lakini Mourinho anadai Manchester ilikuwa timu bora ingawa haikushinda.

“Nawapongeza lakini sidhani kama walistahili kushinda. Nawapongeza. Mimi ni kocha wa Manchester United na inabidi niwe na heshima kwao, sio kwa sababu wao ni timu yangu ya zamani, hapana, ni kwa sababu walikuwa wapinzani wangu leo na nadhani tulistahili kushinda. Nadhani tulikuwa timu bora lakini hivyo ndivyo soka lilivyo,” alisema Mourinho.

“Natamani kujua mtakachosema au kuandika kwa sababu kama timu yangu ingefanya kama ambacho Chelsea imefanya, naweza kufikiria watu wangesema nini. Natamani sana kujua,” alisema Mourinho akiashiria kuishutumu Chelsea kwa kucheza soka la kujihami.

Katika pambano hilo, United haikupiga shuti hata moja katika kipindi cha kwanza lakini ilikuwa bora zaidi katika kipindi cha pili ambapo kipa, Thibaut Courtois alilazimika kufanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa kicha wa Phil Jones. Mourinho anaamini kikosi chake kilimkosa sana mshambuliaji wake wa kimataifa wa Ubelgiji, Romelu Lukaku ambaye alianzia katika benchi kabla ya kuingia baadaye.

“Ilikuwa ngumu kwetu kucheza bila ya Lukaku dhidi ya timu ambayo ilikuwa inajilinda na wachezaji tisa. Unahitaji mchezaji ambaye anasumbua. Chelsea sio wajinga. Wanajua timu yetu bila ya Lukaku au Marouane Fellaini tunakuwa hatuna usumbufu katika mipira ya hewani kwahiyo waliweka watu wanane au tisa kwa ajili ya kudhibiti mipira ya hewani na walitawala.”

“Kila kipigo huwa kinaumiza lakini nakwenda nyumbani nikiwa na hisia kwamba tulijaribu kila tulivyoweza. Sina majuto.”

Kiungo wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka England alienda tofauti na Mourinho ambapo alimpongeza Kocha wa Chelsea, Antonio Conte kwa mbinu zake dhidi ya Mourinho ambazo ziliipa ubingwa wa FA Chelsea.

“Haikufanya kazi kwa Man United lakini inabidi umpe sifa Conte. Timu yake ilikaa sana nyuma na ilinishangaza. Awali nilidhani Chelsea ndio ambao wangemiliki mpira na United wangefanya mashambulizi ya kushtukiza. Lakini Conte alijua hatari kubwa kwa United ilikuwa kasi yao eneo la mbele. Hakukuwa na njia yoyote kwa Sanchez na Rashford kukimbia. Unaweza kusema United walimiliki mpira taratibu,” alisema Scholes.

Scholes pia alimshambulia staa wa United, Alexis Sanchez akimtaka aonyeshe ubora wake huku pia akimpiga kijembe kiungo Mfaransa wa timu hiyo, Paul Pogba.

“Kiwango chake inabidi kiimarike. Hawawezi kwenda chini ya hapo. Nadhani katika mechi chache zijazo za msimu mpya itakuwa muhimu kwake. Anahitaji mashabiki wawe nyuma yake na waamini wataikamata Manchester City. Wanahitaji mchezaji mkubwa,” alisema Scholes.

“Wana wachezaji wakubwa? Paul Pogba hawezi kuwapa ushindi kwa juhudi zake binafsi. Hazard anaweza kufanya hivyo. Alexis Sanchez hawezi, ameonyesha tangu Januari, walidhani angeweza, lakini kwa tulichoona mpaka sasa ni kwamba hawezi.”

“Wanahitaji wachezaji wa kufanya maajabu. Nadhani wana wachezaji wazuri lakini hawajawapata kama Hazard, (Cristiano) Ronaldo, (Lionel) Messi, na najua timu nyingi hazina wachezaji hao.

Leo tofauti ilikuwa Hazard. Tumeliona hilo katika mechi kubwa,” alimaliza.