Mourinho adai anaondoka Man United

MANCHESTER, ENGLAND. SIKU chache tu zimepita tangu ilipoelezwa Manchester United imemwandalia mkataba mpya wa miaka mitano Kocha Jose Mourinho, ambaye ameibuka na kudai ataihama timu hiyo na kwenda kutafuta changamoto mpya kwingineko.

Mkataba mpya ulioelezwa Mourinho atasaini huko Old Trafford umeripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 65 milioni.

Mourinho msimu huu amezidi kuifanya Man United kucheza kwenye ubora wake ikiwa haijapoteza mechi yoyote, huku ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kukusanya pointi 20, mbili nyuma ya vinara, Manchester City, ambao ni mahasimu wao wakubwa.

Wakati akiandaliwa mkataba mrefu, Kocha Mourinho amesema hana mpango wa kudumu Old Trafford hadi anastaafu ukocha kama alivyofanya Sir Alex Ferguson.

Mourinho (54), alisema: “Kitu pekee ambacho naweza kukisema ni kwamba mimi bado ni kocha mwenye mashaka, mipango na malengo ya kufanya mambo mapya. Nina hakika siwezi kumalizia maisha yangu ya ukocha hapa Manchester.”

Kocha Mourinho kwa sasa anapambana na hali yake kutokana na mastaa wake wengi muhimu kuwa majeruhi hasa katika kipindi hiki kikosi chake kikikabiliwa na mechi ngumu ambazo inahitaji kushinda ili kuendelea kuweka hai matumaini yao ya kubeba mataji yote ya msimu huu.

Man United ipo kwenye michuano yote mikubwa ya msimu huu, kuanzia Kombe la Ligi, Kombe la FA, Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.