Nyota Venezuela anyimwa kibali cha kazi England klabu yake ya Watford yashangaa

Muktasari:

Penaranda  aliyeiwezesha Venezuela kucheza fainali ya Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 20, mwezi huu na kufungwa bao 1-0 na England amekuwa akicheza Hispania kwa mkopo kwenye klabu ya Malaga.

Watford, England. Chama cha Soka England (FA) kwa msimu wa pili kimeinyima kibali cha kazi klabu ya Watford kwa kinda wao,  Adalberto Penaranda raia wa  Venezuela.

Penaranda  aliyeiwezesha Venezuela kucheza fainali ya Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 20, mwezi huu na kufungwa bao 1-0 na England amekuwa akicheza Hispania kwa mkopo kwenye klabu ya Malaga.

Kwenye mchezo wa fainali, alikosa penalti na kuiacha timu ya England chini ya miaka  20 ikishinda Kombe la Dunia.

Kijana huyo alijiunga na Watford mwaka  2016  ametolewa mara tatu kwa mkopo.

Kocha wa England, Paul Simpson aliishauri  FA impe kibali cha kazi, lakini amekataliwa kwa madai ya kukosa sifa

Maombi hayo ya kibali kwa raia wa Venezuela yalikataliwa juzi licha ya kung'ara akiichezea nchi yake kwenye Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka  20  nchini Korea Kusini.

Klabu ya Watford imeeleza kusikitishwa na uamuzi huo wa FA kwa mchezaji wao, Adalberto Penaranda ambaye alitarajiwa kuanza kuonyesha makali yake akiwa Ligi Kuu, EPL.

Kocha  Simpson alieleza kuwa Penaranda anao uwezo wa kucheza na kung'ara akiwa England.