#WC2018: Ronaldo aweka rekodi nyingine ya Ulaya, akitupia dhidi ya Morocco

Muktasari:

Katika nafasi tano alizopata kwenye michuano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia, Ronaldo amefanikiwa kuweka kambani mabao manne.

Moscow, Russia. Wakati mchezo wao dhidi ya Morocco ukowa ndio kwanza unaingia kipindi cha pili, tayari Nahodha wa Ureno, mashine ya kupachika mabao, Cristiano Ronaldo, ameshaweka rekodi mpya ya ufungaji mabao kwa bara la Ulaya.

Katika nafasi tano alizopata kwenye michuano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia, Ronaldo amefanikiwa kuweka kambani mabao manne. Hatari! Sio hilo tu, bao lake alililofunga katika dakika ya nne inamfanya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la mapema zaidi kwenye michuano ya mwaka huu.

Kama hiyo haitoshi sasa, Cristiano Ronaldo, mwenye tuzo tano za Ballon d'Or, ameweka rekodi mpya ya Ulaya, kwa kufikisha mabao 85, na kuwa mchezaji pekee aliyefunga mabao mengi zaidi katika mashindano ya kimataifa, yaani amefunga mabao mengi zaodi akiwa na timu ya taifa.

Goli hilo alilofunga kwenye dimba la Luzhinki, katika mchezo wa kundi B, kwa kichwa safi, akiunganisha mpira wa kona, linamaanisha kuwa, amefanikiwa kuvunja rekodi ya zamani ya Straika wa Hungary na Hispania, Ferenc Puskas, baada ya kufikisha mabao 85 katika michezo 152.

Ronaldo alifanikiwa kufikia rekodi ya Puskas, maarufu kama 'Puskas Record'  baada ya kupiga hat-trick kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Hispania, mechi iliyomalizika kwa sare ya 3-3.

Hata hivyo, nyota huyo wa Real Madrid, anashika nafasi ya pili kidunia, na anahitaji kufunga mabao 24, ili aweze kumfikia kinara wa kufumania nyavu, raia wa Iran, ambaye alifunga mabao 109 katika michezo 149 alizoichezea Iran.