#WC2018: Asanteni kwa kuja

Muktasari:

  • Kumekuwa na hisia tofauti kutoka kwa mashabiki na wachezaji wa England huku mastaa wa timu hiyo na kocha wao, Gareth Southgate wakichukuliwa kama mashujaa baada ya kufikia hatua hiyo bila ya kutarajiwa Vyombo vya habari vya England jana vilibeba vichwa vizito vya habari vikiwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la timu yao licha ya kutupwa nje katika michuano hiyo.

MOSCOW, RUSSIA. KELELE za Waingereza zimehitimishwa juzi usiku kule Russia baada ya kuchapwa na Croatia mabao 2-1 kwenye dakika za nyongeza. Sasa wanasubiri pambano la mshindi wa tatu dhidi ya Ubelgiji kesho Jumamosi ili warudi nyumbani.

Kumekuwa na hisia tofauti kutoka kwa mashabiki na wachezaji wa England huku mastaa wa timu hiyo na kocha wao, Gareth Southgate wakichukuliwa kama mashujaa baada ya kufikia hatua hiyo bila ya kutarajiwa Vyombo vya habari vya England jana vilibeba vichwa vizito vya habari vikiwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la timu yao licha ya kutupwa nje katika michuano hiyo. Mara ya mwisho ilifika katika hatua hiyo mwaka 1990 kule Italia.

Beki wa zamani wa England, Gary Neville ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri katika soka alidai timu hiyo imelinyayua soka la England tofauti na fikra za wengi.

“Timu hii imetupeleka katika nafasi ambayo awali hatukudhani kama tungeweza kufika. England haijawahi kufanikiwa kiasi, lakini safari hii imefika nusu fainali. Imelichukua taifa kwa pamoja. Sijawahi kufikiria tungeweza kuona mashabiki wakiwa hivi,” alisema Neville.

“Tulisema kabla ya mechi, vijana lazima watumie nafasi hii kwa sababu huenda isije tena. Ninachotumaini kwa sasa ni inaweza kupata nafasi kama hii tena. Timu za vijana zimeanza kufanya vizuri na kushinda michuano tena. Kwa miaka mingi soka la Kiingereza limekuwa likidharauliwa ndani na nje ya uwanja,” aliongeza Neville

Wakati Neville akizungumza hayo, staa wa mwenzake wa zamani wa Manchester United, Roy Keane alikuwa akibishana na mshambuliaji wa zamani England, Ian Wright huku akiponda kuwa Waingereza walikuwa wanajidai na kuifikiria fainali kabla hawajacheza hata na Croatia.

“Inabidi uwe makini na kuizingatia mechi moja iliyopo mbele yako lakini, kila mmoja alikuwa anaongelea mechi ya fainali kwamba kombe linarudi nyumbani. Sijali nyie kuwa na furaha lakini mlishaanza kujisikia na kupanga mechi ya fainali na jinsi ya kupokea kombe,” aliponda Keane.

Wright alijibu mapigo kwa kusema “Hatukuwa tunaongelea kuhusu fainali hapa, tulikuwa tunakucheka. Ukweli tulikuwa na furaha na hakuwa na furaha kutuona tuna furaha,” alijibu Wright ambaye alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Arsenal.

Kwa upande wa Croatia, staa mahiri na nahodha wa timu hiyo, Luka Modric ambaye aliwahi kucheza England katika klabu ya Tottenham alidai vyombo vya habari vya England vilifanya kosa kubwa kuwapuuza kabla ya mechi hiyo.

“Tulithibitisha mambo tofauti kabisa na kile ambacho watu walikuwa wanaongea kabla ya mechi. Sana sana waandishi wa Kiingereza, wachambuzi wa televisheni. Waliidharau Croatia kabla ya mechi na hilo lilikuwa kosa kubwa,” alisema Modric.

“Maneno yote ambayo waliongea tuliyachukua, tulikuwa tunasoma na kusema ‘Tutaona leo nani atakuwa amechoka’. Kama nilivyosema lazima wawe wapole na kuheshimu wapinzani. Ndivyo ilivyo,” aliongeza staa huyo ambaye kwa sasa anatamba na Real Madrid ya Hispania na Mei mwaka huu alichukua ubingwa wa Ulaya na wababe hao.

Beki wa kulia wa Croatia, Sime Vrsaljko ambaye anakipiga katika klabu ya Atletico Madrid, aliiponda England kwa kudai bado haijabadilika kama ambavyo imekuwa ikisemwa na badala yake imekuwa ile ile ya siku zote huku ikitumia zaidi mipira mirefu.

“Kilichokuwa kinasemwa ni kuwa England hii inatazamiwa upya na imebadili njia yao ya kucheza mipira mirefu, lakini tulipowakaba sana walitumia njia hiyo hiyo. Hawajabadilika,” alisema beki huyo ambaye alisababisha madhara kwa England kwa kupiga krosi ya bao la kwanza lililofungwa na Ivan Perisic.