Vitu 10 vilivyotokea kwa mara ya kwanza England msimu huu

LONDONENGLAND

KUNA mambo hayo yametokea kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kuufanya msimu huu uliomalizika juzi Jumapili kuwa wa kipekee.

1. Chelsea walikuwa mabingwa watetezi wa kwanza kuruhusu kufungwa mabao matatu katika mechi yao ya ufunguzi (Chelsea 2-3 Burnley) na walikuwa wa kwanza kupoteza mechi ya kwanza ya nyumbani wakiwa mabingwa watetezi tangu Aston Villa ilipofanya hivyo Agosti 1981. Mechi hiyo ilikuwa mara ya kwanza pia kwa Chelsea kuwa nyuma kwa mabao matatu hadi wakati wa mapumziko kwenye mechi ya ligi waliocheza Stamford Bridge.

2. Manchester City na Manchester United ndizo timu zilizoshinda timu nyingine zote 19 zilizopo kwenye ligi msimu huu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu zaidi ya moja kufanya hivyo ndani ya msimu mmoja wa Ligi Kuu England.

3. Huddersfield ni timu ya kwanza kuongoza msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi yake ya kwanza tu kwenye ligi hiyo. Timu nyingine iliyowahi kufanya hivyo ilikuwa Norwich City, Agosti 15, 1992. Matokeo hayo yaliifanya Huddersfield kuongoza ligi kwa siku moja.

4. Crystal Palace ilipoteza kwenye mechi saba mwanzoni mwa msimu bila ya kufunga bao lolote, hiyo ni rekodi kwenye Ligi Kuu England. Jambo hilo limeifanya Palace pia kuwa timu ya kwanza kufungwa kwenye mechi saba za mwisho kisha ikabaki kwenye ligi kama ilivyotokea kwa Liverpool msimu 1899-1900.

5. Arsenal imekuwa ya kwanza kwenye Ligi Kuu England kufunga mabao 100 dhidi ya timu moja, ilifikisha idadi hiyo ilipoichapa Everton, Oktoba 2017.

6. Oktoba 2017, Watford ilikuwa timu ya kwanza kwenye historia ya Ligi Kuu England baada ya kufunga mabao ya ushindi kwenye dakika za majeruhi katika mechi tatu mfululizo.

7. Liverpool imekuwa timu ya kwanza kuichapa timu inayonolewa na Pep Guardiola mara tatu tofauti ndani ya msimu mmoja. Ushindi mmoja kwenye Ligi Kuu England na miwili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

8. Liverpool ilishinda kwenye mechi nne mfululizo kwa mabao yanayoanzia manne na kuendelea kati ya Novemba na Desemba 2017, hivyo kuwa timu ya kwanza kwenye historia ya Ligi Kuu England kufanya hivyo.

9. Ni mara ya kwanza pia kwa Tottenham Hotspur kumaliza ligi juu ya Arsenal kwa misimu miwili mfululizo tangu ilipofanya hivyo kwenye misimu ya 1981-82 na 1982-83.

10. Novemba 2017 ilikuwa mara ya kwanza kwa Arsenal kuishinda Burnley kwa bao la dakika ya 90 kwa mara ya tatu mfululizo kwa timu hizo kutokana kwenye ligi ndani ya mwezi huo.