Mtoto wa bosi amtaka akalie kiti cha Wenger, Pep freshi

Tuesday May 15 2018

 

LONDON, ENGLAND

GARY Neville amewaambia hivi Arsenal kama kuna kosa kubwa wanalolifanya basi ni kumwondoa Arsene Wenger huku wakiwa bado hawajampata kocha mwingine wa kurithi mikoba yake.

Tangu, Wenger alipohusishwa na mpango wa kung’atuka na hata alipokuja kutangaza ataachia ngazi mwishoni mwa msimu huu, kuna majina kibao ya makocha yamekuwa yakihusishwa kwenye kukalia kiti hicho cha moto pale Emirates.

Makocha kibao wametajwa kuanzia wenye uzoefu hadi wasiokuwa na uzoefu, akiwamo Mikel Arteta na Patrick Vieira, ambao waliwahi kuwa wachezaji wa Washika Bunduki hao wa London. Max Allegri amegomea fursa hiyo na sasa kura inaonekana kumwangukia Arteta.

Supastaa wa zamani wa Arsenal, Ian Wright, amesema Mhispaniola huyo ndiye mtu mwafaka wa kwenda kurithi mikoba ya Wenger huko Emirates.

Ian Wright haoni kama kuna shida yoyote kumpa Arteta kiti kizito kama hicho hasa ikizingatiwa anakwenda kuirithi timu ambayo ilikuwa chini ya kocha mmoja kwa muda mrefu, ambayo pia hata utamaduni wake ni ule wa kumzunguka kocha huyo.

Anachokiamini gwiji huyo ni kwamba Arteta alikuwa chini ya Wenger, hivyo atakachofanya ni kuendeleza tu falsafa zake kwa sababu si kitu kipya.

Arteta kwa sasa ni Kocha Msaidizi wa Pep Guardiola huko Manchester City. Baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu England Man City msimu huu, Guardiola amesema hawezi kumzuia Arteta kwenda Arsenal kama mabosi wa timu hiyo watahitaji kumpa kazi ya kuchukua mikoba ya Wenger.

Kwa hali ilivyo, Arteta, anaelekea kuwa mteule wa kuchukua mikoba hiyo ya Wenger.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Arsenal, Ivan Gazidis, ameonekana kuunga mkono mpango wa kumpa kazi Arteta kwenda kuwa kocha mpya wa Arsenal.

Jambo hilo linafichua kwamba mpango wa klabu kwa sasa ni kuajiri kocha kijana na kuanza upya mipango yao, huku Vieira naye akiwekwa kwenye mpango huo.

Arsenal inahitaji kocha atakayedumu kwenye timu kwa muda mrefu ili kujenga kikosi imara kama ilivyokuwa kipindi ilipokuwa chini ya Wenger, aliyeinoa timu hiyo kwa karibu miaka 22. Kocha mwingine anayehusishwa kwenye mpango huo ni Luis Enrique.

Taarifa za kutoka ndani ya Arsenal zinaweka wazi kwamba, idadi kubwa ya mabosi kwenye timu hiyo wanahitaji kocha kijana ili kuwafanya kucheza soka la kisasa na kukimbizana na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu England.

Na ndio maana, Gazidis na mkurugenzi mwingine Josh Kroenke, ambaye ni mtoto wa mmiliki Stan Kroenke, wameweka shilingi yao kwa Arteta baada ya kuvutiwa na usaidizi wake Man City.

Kuna kundi jingine la wajumbe wa bodi ya timu hiyo linaloamini kuwa Arsenal inahitaji kuajiri kocha mwenye uzoefu, lakini kwa sababu mpango wa kumleta Arteta unaonekana kusimamiwa na mabosi wakubwa zaidi akiwamo mtoto wa bosi anayemiliki timu, basi Mhispaniola huyo ndiye anayepewa nafasi ya kwenda kumrithi Wenger.