Waganda wafunga pazia la usajili Bandari FC

Muktasari:

Kulingana na Naibu Kocha wa timu hiyo, George Owoko, Bandari haikuwa na mpango wa kumfukuza mchezaji yeyote zaidi ya Waganda hao kundoka baada ya kumaliza mikataba.

KILA lenye mwanzo halikosi mwisho. Ndicho kilichowatokea mastraika Waganda, Musa Mudde na Dan Sserunkuma, ambao hawasajiliwa tena na Bandari FC baada ya kumalizika kwa mikataba yao mwishoni mwa mechi za mkondo wa kwanza wa Ligi Kuu Kenya.

Kulingana na Naibu Kocha wa timu hiyo, George Owoko, Bandari haikuwa na mpango wa kumfukuza mchezaji yeyote zaidi ya Waganda hao kundoka baada ya kumaliza mikataba.

“Ninalopenda kuwafahamisha ni kwamba kamwe hatukumtema mchezaji yeyote lakini wanasoka hao wawili walikamilisha mikataba yao. Ni jambo la kawaida na wanaondoka kwa uzuri tu,” alisema Owoko ambaye pia amethibitisha wamemtoa John Avire kwenda Kakamega Homeboyz kwa mkopo.

Naye kocha wa makipa wa Bandari, Razak Siwa, ameiambia Mwanaspoti kuwa makipa wake; Wilson Obungu na Joseph Okoth, wako katika hali nzuri na watahakikisha hawafungwi bao lolote wanapocheza na Uweza FC kwenye mechi ya GOTV Shield leo Jumamosi.

Siwa alisema Obungu na Okoth wako hali nzuri na alivutiwa mno kwa kuhakikisha hawakufungwa bao kwenye mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Kakamega Homeboyz na Western Stima.

Bandari imepania kuchukua tena taji hilo waliloshinda msimu wa mwaka 2015 kwani maofisa wa benchi la ufundi wana imani kubwa na maandalizi waliyoyafanya. Timu hiyo ilifika Nairobi juzi Alhamisi tayari kwa mchuano huo.