SportPesa yarudisha njaa Kogalo, Ingwe

Muktasari:

Siku ya Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta alitia wino kwenye muswada wa fedha uliyoongeza kodi ya mapato ya kampuni za kubeti kutoka asilimia tano hadi 35.

Kimenuka mwanangu! Ndivyo wasemavyo mitaani. SportPesa wanakwenda zao aise.

Siku ya Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta alitia wino kwenye muswada wa fedha uliyoongeza kodi ya mapato ya kampuni za kubeti kutoka asilimia tano hadi 35.

Hizi ni kampuni kama SportPesa ambao kwa sasa wanafadhili Gor Mahia na AFC Leopards ligi kuu ya KPL, Nakuru AllStars ya daraja la pili miongoni mwa mashirikisho mengine ya spoti.

Sasa wametishia kujiondoa kwenye ufadhili huu kuanzia Januari mwakani kisa, kuongezwa kwa kodi, ambapo hiyo ina maana kuwa kampuni hizi zitatozwa ushuru wa asilimia 65 kwa ujumla; 35 ya mapato na 30 kama kodi ya ushirika.

Katibu wa Wizara ya Fedha, Henry Rotich alipendekeza asilimia ya ushuru kupandishwa hadi 50 ili kupunguza ukuaji wa mchezo wa kamari miongoni mwa vijana ndani ya mazingira magumu. Hata hivyo, Bunge liliangalia pendekezo hilo na kupunguza hadi asilimia 35.

Afisa Mtendaji Mkuu wa SportPesa, Ronald Karauri tayari ametuma onyo kwa vilabu vinavyotegemea mapato ya kampuni hiyo kuu hapa nchini.

“Kama SportPesa, tunapanga kuandikia vilabu na mashirika kwamba, kuanzia mwezi Januari tutaondoa udhamini wote. Kulingana na muswada mpya kuanza kazi Janauri, tunataka washirika wetu kujipanga vilivyo.

“Gharama zetu za kufanya biashara kama kampuni zitaathirika sana na hivyo, tunapaswa kuzingatia athari za uendeshaji badala ya ushirikiano,” alisema.

Inachomaanisha ni kwamba Gor na Leopards hawatapokea Kshs. 60 na Kshs. 45 milioni wanazokula kutoka SportPesa kwa mwaka sawia na Kshs. 500 milioni za kampuni hiyo kwa KPL.

Ni maamuzi yatakayorejesha timu hizi miaka miwili iliyopita walipokuwa wakiteseka na njaa na kushindwa kulipa mishahara wachezaji.