Skendo za Olimpiki kimeumana upya

Muktasari:

  • Arap Soi, ambaye ni Ofisa wa Polisi ameshutumiwa kwa kidikteta ikiwa pamoja na kuwapa wanariadha malazi mabovu, kunyima makocha tiketi na badala yake kuwafadhili watu wa karibu wakiwemo wanawake, ambao wanadaiwa ni mpango wa kando.

KENYA imefanya vizuri kwenye michezo ya Olimpiki 2016 iliyofanyika jijini Rio De Janeiro, Brazil, lakini mafanikio hayo yamefunikwa na rundo la skendo ambazo kwa hakika zimewachosha Wakenya.

Kila kukicha skendo mpya zimekuwa zikiibuka juu ya kilichotokea Rio na sasa, sekeseke hilo linaendelea kufukuta baina ya serikali na vigogo wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOCK).

Lawama nyingi zinaelekezwa kwa viongozi wa NOCK na Waziri wa Michezo, Dk. Hassan Wario, ambao wanadaiwa kula bata walipokuwa Rio badala ya kushughulikia wanamichezo.

SKENDO ZA RIO

Kashfa hizo zinaangaziwa sana kwenye vyombo vya habari, zilimtikisa kila moja hata Rais Uhuru Kenyatta akiwa kwenye kile kiti chake cha dhahabu katika Ikulu ya Nairobi.

Mwenyewe wakati akiwatumia ujumbe wa kuwapongeza wanariadha waliotuletea fahari, aliahidi kuhakikisha viongozi wote wa NOCK waliohusika na usimamizi mbaya wakiongozwa na Chief De Missione Stephen Arap Soi, aliyeongoza ujumbe huo watachukuliwa hatua. Arap Soi, ambaye ni Ofisa wa Polisi ameshutumiwa kwa kidikteta ikiwa pamoja na kuwapa wanariadha malazi mabovu, kunyima makocha tiketi na badala yake kuwafadhili watu wa karibu wakiwemo wanawake, ambao wanadaiwa ni mpango wa kando.

Mwanariadha wa Marathon ambaye ni mbunge wa Cherengany, Wesly Korir ametumika kuianika NOCK, akiwalaumu kwa kumsababishia ashindwe kumaliza mbio zake kwa kumpa maji mabaya, kushindwa kuwakatia tiketi kwa wakati baadhi ya wanaridha kufuatia kumalizika kwa Olimpiki hali iliyowapeleka wanariadha hao kuishi katika hali duni kwa siku nne kwenye mitaa ya mabanda kule Rio wakisubiria tiketi za ndege.

Aidha aliishutumu NOCK kwa kuuza jezi za wanaridha zilizotolewa na kampuni ya Nike ambapo, kila mchezaji alitakiwa kupewa nane lakini wakaishia kupata moja huku zingine zikitoweka.

Hii ni baadhi tu ya kashfa hizo inayojumulisha pia kutimuliwa kwa kocha John Anzrah kutokana na uzembe wa NOCK kushindwa kumtafutia pasi na bingwa wa Marathon Eliud Kipchoge kukosa kulakiwa na maafisa wa Team Kenya katika Uwanja wa Ndege alipowasili Rio, usiku kushiriki mbio hizo na kulazimika kumfuata Stephen Rotich wa Uganda.

NOCK YAVUNJWA

Skendo hizo zilizua tumbo joto hasa kutoka kwa umma na Alhamisi baada ya Dkt. Wario, ambaye alijiondoa lawamani kuwa hakuwa na uwezo wa kufanya lolote kwa kuwa NOCK ni chombo huru, aliitisha kikao na kutangaza kukivunjilia mbali chombo hicho. Ghafla baada ya kuona maji yanamfika shingo, Dkt Wario alisahau kauli yake ya awali kuwa hana mamlaka ya kuingilia utendaji kazi wa NOCK, kwa kuivunjilia.

Kisha majukumu ya chombo hicho aliyahamishia Sports Kenya, lakini Katibu Mkuu wa NOCK, Francis Paul amesisitiza kuwa hawawezi kung’atuka na chombo hicho ni huru na ni IOC pekee yenye uwezo wa kuwasimamisha kazi.

“Sifikiri kama waziri ana mamlaka ya kuivunjilia mbali NOCK. Hatua kama hiyo huchukuliwa kama usumbufu kutoka kwa serikali na taifa linaweza kuishia kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya Olimpiki. Hiki ni chombo huru na hakuna aliye na mamlaka ya kutuondoa madarakani,” alisema Paul.

IOC YATOA SAUTI

Huku hatua yake hiyo Wario ikiendelea kuzua hisia mseto wengi wakifurahia, huku maofisa wa NOCK wakisema watagadia ofisini, IOC nayo imeanza kuichunguza NOCK kuhusiana na skendo hizo. IOC inaendeshwa na sheria na kanuni kama zilivyo za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), ambapo serikali haipaswi kuingilia usimamizi wake ngazi ya kitaifa. Serikali inayokiuka agizo hilo hupigwa marufuku kushiriki mashindano ya Olimpiki.

Bado IOC haijatoa uamuzi wake kuhusiana na Kenya, baada ya serikali kuivunjilia mbali NOCK. Hata hivyo, chombo hicho kimesema hakitafanya pupa kuichukulia Kenya hatua mpaka pale kitakapokamilisha uchunguzi wake.

Katika taarifa yake IOC imesema imeona sababu za serikali kuvunjilia mbali NOCK na kwamba, inaendelea kufanya uchunguzi kabla ya kutangaza uamuzi wake.

Kwenye mashindano hayo David Rudisha, Faith Kipyegon, Vivian Cheruiyot, Conseslus Kipruto, Eliud Kipchoge na Jemima Sumgong walitwa dhahabu, nao Vivian Cheruiyot, Paul Tanui, Hyvin Jepkemoi, Boniface Mucheru, Julius Yego na Hellen Obiri wakitwaa nishani ya fedha huku Margaret Nyairera akiishindia taifa nishani ya shaba.