Sinema ya Marian, Ingwe yafika patamu

Saturday June 24 2017

 

By THOMAS MATIKO

Acha sinema iendelee. Kocha Mromania Dorian Marin aliyetimuliwa pale AFC Leopards baada ya kufanya kazi kwa siku 14 tu tangu alipoteuliwa, sasa kawapigia magoti mabosi wa klabu hiyo akiwaomba wamrejeshe kazini.

AFC ilimtimua kazi Marin siku nne zilizopita baada ya kumleta kurithi mikoba ya Stewart Hall aliyejiuzulu wadhifa huo baada ya kuiongoza Ingwe kwenye mechi 13 tu.

Lakini, Marin hajaweza kudumu pale akifungishiwa virago vyake baada ya kusimamia mchuano mmoja pekee wa KPL dhidi ya Mathare United ulioishiwa kwa sare tasa wikendi iliyopita.

Madai ya kutimuliwa kwa Marin aliyefika na kuifuata timu kule Dar, Tanzania ilipokuwa ikishiriki dimba la Sportpesa Cup zilitolewa na uongozi wa klabu uliosema kuwa walifikia uamuzi wa kumfurusha kwa kushindwa kuelewana na bechi lake la ukufunzi na vile vile wachezaji.

Hata hivyo, Marin ambaye bado yupo nchini kwa kile kinachoelezwa ni jitihada za kubembeleza viongozi wamrejeshee kazini, kakanusha madai hayo.

Kulingana naye, sio kweli kwamba kashindwa kuwa na uhusiano mwema na benchi lake la ukufunzi au wale wachezaji.

“Madai yaliyotolewa sio, ukweli wa mambo ni kuwa kuna baadhi ya wanakamati wa bodi kuu ya klabu wasionipenda, wananichukia na sielewi ni kwa nini. Hao ndio walioichochea benchi langu la ukufunzi pamoja na baadhi ya wachezaji kunikataa. Sijawahi kuwa na tatizo na mtu yeyote pale,” Marin ameitiririkia safu hii.

Kocha huyo kaahidi kuitisha kikao cha wanahabari juma lijalo kabla hajaondoka nchini endapo atashindwa kuafikiana na Ingwe, ili kutibua kiini cha ugomvi huo.

Marin kawarai viongozi wanaomkata kumpa fursa tena klabuni humo ili aweze kuonyesha uwezo wake.

“Natamani sana kuwafunza vijana wale, na kuwatengeneza waweze kucheza soka la Ulaya, ndio kitu nafsi yangu inakusudia kufanya ukizingatia kuwa niliicha kazi nzuri kule Syria kuja huku,” Marin akaongeza.

Kwa sasa wadhifa wake huo umechukuliwa na kocha wa zamani wa Muhoroni Youth, Tom, Juma aliowaongoza kutwaa kombe la Top 8 mwaka jana walipowabandua mibabe Gor Mahia fainalini.

Huku kisanga ya Marin kikiendelea kukishangaza mashabiki wa Ingwe, ikimbukwe kuwa rekodi yake ya kudumu pale AFC kwa siku 14 ni bora zaidi kuliko ya kocha wao wa zamani Mreno, Vitor Salvado, aliyeteuliwa na kufutwa kazi kesho yake kwa misingi kwamba hakuwa amehitimu ukocha.