Sababu za Aucho kukwama Ulaya

AUCHO

Muktasari:

  • Hata hivyo, baada ya kushindwa kunasa dili hilo, Aucho aliibukia Afrika Kusini na kusaini kuichezea Baroka FC, ambapo sababu zimetajwa kuwa ni kuchemsha kufikia viwango.

KIUNGO wa nguvu aliyekuwa na jina kubwa na tegemeo pale Kogalo, Mganda, Khalid Aucho, ameshindwa kunasa dili la kucheza soka la kulipwa Ulaya na sasa ameibukia klabu ya Baroka FC pale Afrika Kusini.

Awali, Aucho alikuwa akifanya majaribio kwa zaidi ya miezi miwili katika klabu ya Aberdeen  ya Scotland, ambapo ilitarajiwa angefuata nyayo za Mkenya, Victor Wanyama aliyeanzia Celtic na baadaye kutua England na sasa anatamba na Tottenham Hotspurs.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kunasa dili hilo, Aucho aliibukia Afrika Kusini na kusaini kuichezea Baroka FC, ambapo sababu zimetajwa kuwa ni kuchemsha kufikia viwango.

Pia zipo sababu kuwa Kogalo ilitaka kulipwa dau kubwa ili kumwachia kiungo huyo mwenye ustadi wa kukaba na kusambaza mipira ya mwisho kwa mastraika.

Licha ya kuwa kwenye ubora wa juu kabisa pale Kogalo, lakini imebainika kuwa Aucho alichemsha katika zoezi la kufanya shambulio la kushitukiza (Counter attack).

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, imeelezwa kuwa Aucho alishindwa kujiunga na Aberden kutokana na kushindwa kumridhisha kocha, Derek Mclness.

“Kocha Derek aliwaagiza wachezaji wake wote wapya aliokuwa akiwafanyia majaribio kushiriki zoezi la kufanya shambulizi la kushtukiza (kupiga kaunta).

“Kila mmoja alitakiwa kuchukua mpira kutoka katikati mwa uwanja, atimke nao kwa mita kadhaa kwenda goli la wapinzani kisha atoe pasi ya bao kwa mchezaji aliye kwenye nafasi ya kufunga, au apige shuti. Lakini Aucho hakuweza,” ilielezwa.

Pia, gazeti hilo lilimnukuu Mclnness akimsifia Aucho licha yake kushindwa kumridhisha kwenye majaribio hayo kama ilivyotarajiwa.

“Kwa kile tulichokiona kwake, ni mchezaji mwenye uwezo ila sio wa sampuli ya kufikia ubora tulionao kwa sasa,” alisema Mclnness.

Aucho anafahamika kuwa kiungo asiye na kasi ila mzuri sana katika kuzima mashambulizi na usambazaji mipira. Mchango wake timuni ulichangia Gor kutwaa ubingwa wa ligi kwenye misimu miwili iliyopita na kuondoka kwake kumetajwa ni sababu ya Gor kusua sua na kupoteza makali uwanjani.