Rudisha sio wa mchezo mchezo

Muktasari:

Mbio hizo za mchujo zilianza jana Ijumaa katika uwanja wa Nyayo kusaka kikosi cha taifa kwenye shindano la World Championships 2017 zitakazofanyika baadaye Agosti, mwaka huu kule London, Uingereza

Licha ya Shirikisho la riadha nchini, AK kuondoa mpango wa ‘Wild Card’ baadhi ya mastaa wanariadha walichunia mbio za mchujo kusaka kikosi kitakachokwenda London, Agosti mwaka huu.

Mbio hizo za mchujo zilianza jana Ijumaa katika uwanja wa Nyayo kusaka kikosi cha taifa kwenye shindano la World Championships 2017 zitakazofanyika baadaye Agosti, mwaka huu kule London, Uingereza.

AK ilisema imefutiliwa mbali mpango wa Wild Card ambao ni uteuzi wa moja kwa moja kuunda Team Kenya kwa wanaridha mabingwa watetezi. Hata hivyo, AK imejikuta ikipindisha sheria yake hiyo mpya na kuwaruhusu baadhi ya mastaa kuunda timu licha ya wao kuzichunia mbio hizo za mchujo.

David Rudisha, mfalme na mshikilizi wa rekodi ya mbio za mita 800 duniani anaongoza listi ya wanaridha saba waliopewa Wild Card na hawatashiriki mbio za mchujo licha ya kutakiwa wafanye hivyo.

“Nimeiomba uongozi iniruhusu nisishiriki mbio za mchujo kwa sababu ndio nimerejea nchini hivi majuzi,” Rudisha alisema aliyetokea ughaibuni ambako amekuwa akishiriki mashindano mbalimbali ikiwemo ile ya ‘Salute The Legend’ kule Jamaica iliyoandaliwa kumwaga Usain Bolt atakayestaafu baada ya ngoma ya kule London.

Pia, nguli wa mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji, Ezekiel Kemboi hatashiriki kwa kuwa ndiye bingwa mtetezi. Naye pia kapewa Wild Card.

AK imesisitiza kuwa hata kama mwanaridha ana Wild card lazima ashiriki mbio za mchujo ila imeonekana kulegeza msimamo huo.