Neema kuiangukia Ligi Pwani Kusini

Thursday September 7 2017

Kikosi cha Coast Stima FC kinachoendelea kuwika

Kikosi cha Coast Stima FC kinachoendelea kuwika katika Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza kabla ya mechi mojawapo yao uwanja wa nyumbani wa Mbaraki Sports Club. 

By ABDULRAHMAN SHERIFF, MOMBASA

KLABU zinazoshiriki Ligi ya Pwani Kusini zinatarajia kupata afuweni ya gharama ikiwa matarajio ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) tawi la sehemu hiyo litafanikiwa kupata udhamini wa ligi hiyo.

Akitangaza habari njema hiyo kwa klabu za mkoani, Mwenyekiti wa FKF Pwani Kusini, Gabriel Mghendi alisema wana matarajio makubwa ya kupata mdhamini wa ligi hiyo na akazitaka klabu ziendelee kudumisha nidhamu ili kuvutia wadhamini hao.

“Kuna matumaini makubwa kwa klabu zinazoshiriki ligi hii kupata udhamini kuzipunguzia gharama,” alisema Mghendi.

Ni klabu za matawi madogo ya FKF ya Kaunti za Taita Taveta, Kwale na Mombasa na Kaunti Ndogo ya Kaloleni ndizo zinazoshiriki ligi hiyo.

Mghendi ametangaza Ligi ya Pwani Kusini la Soka la wanawake inatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu na klabu 20 zinatarajia kushiriki.

“Tunataka klabu za soka la wanawake zijitokeze kushiriki,” alisema Mghendi.

Timu mbili za Mkoa wa Pwani za soka ya wanawake zinashiriki Ligi Kuu ya Kenya. Timu hizo ni Spedag Ladies FC na Mombasa Olympic Ladies, iliyo na wachezaji wengi waliokamilisha shule za upili mwaka jana.

Spedag ina wachezaji tisa wa timu ya Taifa ya Harambee Starlets lakini wengi wao wanaishi Nairobi na miji jirani. Olympic ina wanasoka watatu wa timu ya Yaifa ambao ni Mwanahalima Adam, Winfred Achieng na Gererder Akinyi.