Mombasa Olympic yapotea Nairobi

Muktasari:

Kocha Mkuu wa Makolnders, Michael Okanga aliambia Mwanaspoti kuwa walijipanga kuja Mombasa kuvunja rekodi ya Olympic ya kutoshindwa. “

TIMU ya Mkoa wa Pwani inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka la Wanawake, Mombasa Olympic  imetoa matokeo mabaya kwa kupoteza rekodi yake ya kutoshindwa ilipofungwa mabao 3-1  na wageni wao kutoka jijini Nairobi, Makolanders Ladies FC.
Kocha Mkuu wa Makolnders, Michael Okanga aliambia Mwanaspoti kuwa walijipanga kuja Mombasa kuvunja rekodi ya Olympic ya kutoshindwa. “Haikuwa bahati ushindi wetu kwani tulipanga namna ya kuwashinda na wachezaji wakafanya na tukapata pointi zote tatu,” akasema.
Naye Kocha Mkuu wa Olympic, Joseph Oyoo alisema Michezo ya Shule za Upili yaliyokuwa yakifanyika mjini Mombasa na baadhi ya wachezaji wake kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan pamoja na kutofanya mazoezi kuwa sababu ya timu yake kupoteza mchezo huo.
“Nina imani kubwa kwa kuwa sasa michezo hiyo imemalizika na tutapata fursa ya kujiandaa kwa mechi yetu ifuatayo, sina wasiwasi tutarudia hali yetu ya kushinda kama tulivyoanza ligi hiyo,” akasema Oyoo.
Kwa niaba yake na wachezaji wenzake, Nahodha wa Olympic Gererder Akinyi aliwaomba msamaha mashabiki kwa kushindwa kupata ushindi katika mechi hiyo akifahamisha kuwa kulikuwa na sababu kadhaa za timu kutokuwa katika hali nzuri.
“Wachezaji wetu walikuwa wamechoka kutokana na kushiriki kwenye mechi za shule na pia wengine kuwa wanafunga saumu. Lakini tunawaahidi kwamb watafurahika tutakapocheza mechi zijazo,” akasema Gererder.