Modern Coast yapania kufanya kweli

Saturday July 1 2017

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF, MOMBASA

MODERN Coast Rangers FC imepania kuzikomoa timu pinzani zitakazokumbana nazo kwenye mechi za mkondo wa pili kwani inatamba baada ya kuwasajili ‘majogoo’ watano wakiwemo wanne kutoka klabu za Ligi Kuu ya SportPesa.

Katibu wa Rangers, Ferdinand Ogot alikuwa jijini Nairobi hapo jana kuhakikisha hati za sajili zao hizo mpya zimeidhinishwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) akiamini wanasoka hao watano watakipa kikosi chake nguvu mpya.

Kulingana na Ogot, wanasoka wao wapya waliowasajili kutoka klabu za ligi kuu ni Dennis Owino (Chemelil Sugar), Abdul Main (Sofapaka), Eliakin Nyanga (Kariobangi Sharks) na sajili ya mkopo Harun Pamba kutoka Mathare United.

Mchezaji mwingine aliyesajiliwa kutoka klabu ya Supaligi ya Taifa ni Dominic Waithaka kutoka Savannah FC ambayo inashiriki ligi sawa na Rangers. “Wanasoka hawa ni wazuri na nina hakika timu tutakazokutana nazo zitapata kichapo cha mbwa,” akasema Ogot.

Katibu huyo alithibitisha kuwa straika wao Francis Ocholla ametia saini ya kukichezea klabu cha Sofapaka kwa kipindi cha miaka miwili. Habari kutoka Sofapaka inafahamisha Mwanaspoti kuwa Ocholla yuko kambini akijitayarisha kwa mechi dhidi ya Nakumatt hivi leo.

Kulingana na Ogot, wamewatema wachezaji watano na kuwapa barua za kuwaruhusu kuchezea klabu wazipendazo. Wanasoka hao waliotemwa ni Nelson Mganga, Collins Ouma, Athman Mzee, Edmarn Adard na Erick Okoth.