Mechi hii ni vita ya Daudi na Goliati

Muktasari:

Vumbi ametoa ahadi ya timu yake kujitahidi iwezavyo kuibuka washindi  kwenye patashika hiyo akisema hawatetemeshwa na ule ukweli kwamba Tusker ndio mabingwa wa soka nchini.

KOCHA, Amin Vumbi, wa SS Assad FC anaamini kuwa mechi yao ya raundi ya kwanza ya shindano la GOTV Shield dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Kenya, Tusker FC, itakuwa pambano kati ya ‘Daudi na Goliati’.

Vumbi ametoa ahadi ya timu yake kujitahidi iwezavyo kuibuka washindi  kwenye patashika hiyo akisema hawatetemeshwa na ule ukweli kwamba Tusker ndio mabingwa wa soka nchini.

Anasema kamwe hawatishiki na jina kubwa la wapinzani wao kwani anaamini vijana wake watacheza bila ya wasiwasi wowote.

Mkufunzi huyo anayejulikana kwa jina maarufu la Mara, ameliambia Mwanaspoti kuwa wana hamu kubwa ya kuwashitua wapinzani wao kwenye mechi hiyo  ambayo itafanyika uwanjani Mbaraki Sports Club kesho Jumapili.

“Mechi yetu itakuwa baina ya ‘David na Goliath’ na nawaomba mashabiki wa soka wa Mkoa wa Pwani waje uwanjani kwa wingi kutushangilia. Tunatambua Tusker ni timu kubwa, lakini vijana wangu wako tayari kuingia uwanjani na kuhakikisha wanatekeleza kazi yao ipasavyo,” alisema Vumbi.

Mkufunzi huyo aliyeisaidia Ramisi Secondary kushinda kombe la soka kwenye Michezo ya Shule za Upili ya Mkoa wa Pwani, anasema ingawa wanasoka wengi wanafunga saumu, lakini watakabili wapinzani kwa kiwango cha juu.