Libby; Mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni

Libby

Muktasari:

  • Ni nani binti huyo? Si mwingine bali ni Ambundo Klement ‘Libby’ anayelenga kutingisha jukwaa la burudani ya muziki kuanzia Kenya hadi duniani kote.

ANAAMINI ana uwezo wa kutosha wa kujituma kufanya kazi nyingi  na kutimiza malengo yake kwenye masuala mbalimbali.

Kwa mtazamo wake hili linapigwa jeki vilivyo na familia yake inayompa ushirikiano katika kazi zote afanyazo.

Ni binti mcheshi, mwenye sauti nyororo na tabasamu la kuvutia si haba. Kadhalika ni kati ya wanamuziki ambao pia ni wataalamu wa mitindo ya mavazi, hivyo ana matumaini makubwa ya kupata mafanikio kupitia sanaa.

Ni nani binti huyo? Si mwingine bali ni Ambundo Klement ‘Libby’ anayelenga kutingisha jukwaa la burudani ya muziki kuanzia Kenya hadi duniani kote.

Ingawa hajafanya kazi nyingi katika utunzi wake, video ya kibao  ‘Rusha Mkono’ ndiyo inayomtambulisha vizuri kwa mashabiki ambao hakika wanapagawishwa vilivyo.

Libby kama aitwavyo na mashabiki wake, alianza kujihusisha na masuala ya uimbaji akiwa katika umri wa miaka saba kwa kuanza kuimba nyimbo za wasanii wakali na kushiriki kwaya pia.

“Lakini nilijitosa katika ulingo wa burudani ya kibiashara karibu miaka mitatu iliyopita. Ni baada ya kujiridhisha kuwa ninao uwezo mkubwa wa kuimba,” anasema.

“Niliutambua uwezo wangu kutokana na mafanikio makubwa ya kuimba kwaya kanisani. Ndipo nikafikia hatua ya kukata shauri ya kuufanya muziki kuwa ajira yangu.”

Anasema baada ya kukata shauri, ni kama Mungu alimsikia na kumpa baraka yake.

“Haikuchukua muda nikakutana na mmiliki wa studio ya GrandPa Records (Refigah). Yeye alinifanyia mipango ya kurekodi na pia aliniunganisha na msanii Sonia, hivyo ndivyo mambo yalivyooanza,” anasema.

Anakiri kuwa nyota yake ilizidi kumwakia kwani alipata msaada mkubwa wa ushauri kutoka kwa wasanii wengi waliompa motisha ya kujibidiisha jambo ambalo anazidi kulitilia mkazo.

Baada ya kushirikishwa katika nyimbo kadhaa za wengine, Libby akaamua kutoa cha kwake miaka miwili iliyopita, kinaitwa ‘Fimbo ya Kwanza’. Hapo aliwanasa mashabiki kwa sauti yake mwanana ya kumtoa nyoka pangoni.

Mafanikio ya wimbo huo yamemzawadia mkataba wa miaka miwili na GrandPa Records inayosimamia kazi ya kurekodi na kusambaza nyimbo zake.

Hatua hiyo imemwezesha kujiunga na familia ya wanamuziki kadhaa wakiwamo mwanadada aliyewahi kushiriki shindano la Tusker Project Fame (TPF), Amileena. Wengine ni Pizo Dizo, DNA, Kidis na wengineo.

Anasema kila siku kwake ni mafunzo. Hivyo anawavulia kofia wanamuziki kadhaa wa Afrika Mashariki wakiwamo, Hussein Machozi na Mr. Blue (Tanzania) pamoja na HB Toxic na Cindy Sanyu (Uganda) anaosema kazi zao ni nzuri kwa mpangilio wa vyombo na sauti bila kusahau mawaidha kwa jamii.

Hata hivyo anasema bado hajaridhishwa na namna serikali inavyouchukulia muziki. Anashauri fani hiyo ithaminiwe zaidi ili kuwanufaisha wahusika na jamii kwa ujumla.

Hakuna lisilo na changamoto. Kwake anasema Wakenya hawana budi kuonesha ari ya kuijenga sekta hiyo kusudi kuinua watunzi wa hapa nchini.

“Ni jambo la kutia hofu sana kuona Wakenya wenzetu wanapenda kazi za muziki wa kigeni na kuzipuuza za muziki wenyeji. Lazima kuibadili hali hii,” anasema.

Mrembo huyu si mchoyo wa ushauri. Anawasihi wasanii wapya kujituma kufanya kazi zao kwa kujiamini kwani hakuna lililo zuri lisilo na ugumu, anasema la msingi ni kujipa mwelekeo.

“Pia nawaomba wenzangu, tutambue kuwa umaarufu ni mtego wa maisha, tukae mbali na mambo ya dawa za kulevya,” anasema.