Lewa Marathon: Babu Gituchi aweka rekodi mpya

Muktasari:

  • Babu Gituchi, kama anavyofahamika na wengi kwenye mbio hizo, amekuwa akishiriki mbio hizo tangu yaanzishwe mwaka 2000, akishiriki mbio za nusu marathon, akiwa amevaa nambari ya ushiriki 1398, alimaliza mbio hizo, akitumia muda wa saa 3:22:30.

Isiolo, Kenya.  Mwanaridha wa muda mrefu, Babu John Rwengo Gituchi, ameweka rekodi ya kuwa mwanariadha mkongwe zaidi kuwahi kushiriki mbio za hisani za Lewa Marathon, yanayofanyika kila mwaka katika hifadhi ya wanyama ya Lewa, baada ya kumaliza makala ya 19, akiwa na umri wa miaka 88.

Babu Gituchi, kama anavyofahamika na wengi kwenye mbio hizo, amekuwa akishiriki mbio hizo tangu yaanzishwe mwaka 2000, akishiriki mbio za nusu marathon, akiwa amevaa nambari ya ushiriki 1398, alimaliza mbio hizo, akitumia muda wa saa 3:22:30.

Akionesha kufurahia kumaliza mbio hizo huku akiwa ngangari kinoma, Babu Gituchi, aliiambia Mwanaspoti Digital kuwa, anatazamia kuendelea kushiriki mbio hizo hadi pale miguu yake itakaposema basi.

“Mungu ni mwema, nasikia kwa sasa mimi ndio mwanariadha mkongwe zaidi anayeshiriki mbio hizi. Kama unavyoona bado niko fiti, mwakani nitakuwa hapa, nitakimbia hadi miguu iseme basi,” alisema Babu Gituchi.

Mbio za Lewa Marathon, hufanyika kila mwaka kwa udhamini mkubwa wa kampuni ya simu ya Safaricom, kwa ushirikiano na hifadhi ya wanyama ya Lewa, lengo kuu ikiwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watu wenye hitaji katika jamii.

Tangu mwaka 2000, ambapo mbio za kwanza zilizpofanyika, Lewa Marathon, imekuwa ikifahamika kote duniani kutokana na ugumu wake, hasa hali ya hewa isiyotabirika, njia zisizoeleweka na washiriki wakubwa katika medani ya riadha.

Baadhi ya majina makubwa kuwahi kushiriki mbio hizi ni mshindi wa fedha katika michezo ya Olimpiki, mwaka 2004, Catherine Ndereba na Rais wa Kamati ya Olimpiki (NOCK), Paul Tergat.