Kocha wa Tusker maji yamfika shingoni

Saturday September 16 2017

 

By Na THOMAS MATIKO

Nairobi. Mfa maji haachi kutapata. Lazima tu atapambana angalau kujaribu kujinusuru asizame majini. Ndio hali anayopitia kwa sasa Kocha George Nsimbe wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Kenya, Tusker FC.
Ni wazi kwamba Nsimbe anatapatapa. Licha ya dalili zote kuashiria kwamba itakuwa vigumu sana kwa Tusker  wanaochechemea, kutetea ubingwa wao msimu huu, kocha huyo kashikilia kuwa bado wana fursa na kwamba hajakataa tamaa.
Kwa sasa Gor wapo kileleni kwa pointi 50 huku wakiwa  na mechi moja kibindoni. Kwa upande wa Tusker ambao vipigo vimekuwa ndio mpango mzima, wametulia katika nafasi ya nane kwa alama 33 ingawaje pia nao wana mechi moja ya ziada.
Ushindi wa juzi katika mwa juma walipowatandika Zoo Kericho  2-1 ndio  matokeo yanayoonekana kumpa nguvu Nsimbe ya kuamini kwamba bado wana fursa ya kukimbizana na Gor  msimu huu.