Nsimbe hana chake Tusker

Muktasari:

 “Unajua ni komenti ambazo hazikuchukuliwa vizuri na wachezaji ndio maana tukaketi naye kuelewana akae kando na timu,” alisema Mwenyekiti wa Tusker, Dan Aduda.

KOCHA Mganda George ‘Best’ Nsimbe ameombwa kukaa kando katika kikosi cha Tusker hadi mwisho wa msimu. Naibu wake Francis Baraza ataongoza timu hiyo kwenye mechi nne zilizosalia akisaidiwa na kocha wa academia, Leonard Odipo.
 “Unajua ni komenti ambazo hazikuchukuliwa vizuri na wachezaji ndio maana tukaketi naye kuelewana akae kando na timu,” alisema Mwenyekiti wa Tusker, Dan Aduda.
Taswira kamili ni kwamba ilikua njia tu ya kumfuta kazi Nsimbe na si mara ya kwanza kwani, imekua rekodi ya Tusker kuwafuta kazi makocha wasioshinda mataji.
Mwaka 2015, Francis Kimanzi aliombwa kuketi kando mechi tano kabla ya msimu kutamatika kwa sababu ya kung’olewa kwenye Ngao ya GOtv na kukosa kutetea taji la Nane Bora. Msimu ulipokwisha, akatemwa.
Mwaka 2013, kocha Robert Matano alifurushwa kwa kukosa kutetea taji la ligi msimu huo, akishinda kombe la nane bora tu na Oktoba 2012, Sammy Pamzo Omollo akafutwa kazi kwa matokeo mabovu mechi chache kabla ya msimu kuisha.
Matano alichukua nafasi hiyo na kuongoza Tusker kunyakua ubingwa wa 2012 kisha mwaka 2010, James Nandwa alitupiwa virago pia katikati ya msimu kwa kukosa kushinda mechi licha ya kuwa na kikosi thabiti.