Kocha Dylan Kerr awatetea wachezaji wake

Muktasari:

Mkufunzi Kerr kadai kuwa wachezaji wake wamechoka kinoma na wanahitaji kupumzika vyema kabla ya kukutana na Waarabu huo ikiwa ni baada ya kibarua cha dimba la CAF walikosafiri ugenini Madagascar kwa mechi ya marudiano dhidi ya Leones Vegetarianos na mara tu  waliporejea, siku tatu baadaye wakakutana na Kariobangi Sharks kwenye mechi ya ligi kuu.

KOCHA wa Gor Mahia, Dylan Kerr amewacharukia mabosi wa  KPL kwa kuwakaushia siku kadhaa za mapumziko ili waweze kujiaandaa vyema kukabiliana na Esperance kwenye dimba la uwaniaji wa kombe la CAF Champions League.

Mkufunzi Kerr kadai kuwa wachezaji wake wamechoka kinoma na wanahitaji kupumzika vyema kabla ya kukutana na Waarabu huo ikiwa ni baada ya kibarua cha dimba la CAF walikosafiri ugenini Madagascar kwa mechi ya marudiano dhidi ya Leones Vegetarianos na mara tu  waliporejea, siku tatu baadaye wakakutana na Kariobangi Sharks kwenye mechi ya ligi kuu.

Gor wanakutana na mababe hao wa Tunisia Jumatano ijayo uwanjani Machakos kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya mechi za mchujo, kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya dimba hilo.

Kogalo ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini walifuzu raundi ya kwanza ya mchujo baada ya kuwalima Leones Vegetarianos wa Madagascar magoli 2-0 nyumbani na kisha kulazimisha sare ya 1-1 ugenini.

Mechi ya pili ya mchujo imeratibiwa na CAF kuchezwa katikati mwa juma lijalo  hali iliyowaweka Gor pabaya ikizingatiwa kuwa  pia  kwa wakati huo wanashiriki ligi kuu inayoendelea wanakopambana kutetea taji lao.

Kutokana na hali hiyo Kogalo wamejikuta wakiwa na ratiba finyu inayowalazimu kucheza mechi tatu za ligi kuu katika kipindi cha wiki moja kabla ya kukutana na miamba  hao wa Kiarabu Esperance wenye uzoefu na tajriba kubwa katika dimba la CAF Champions League  walilofanikiwa kushinda mara mbili katika historia ya mashindano hayo.