Kipruto, Kamworor watema shombo

Muktasari:

Ikiwa imesalia mwezi mmoja tu kabla ya shindano hilo kuanza kule London, England, wanariadha wazalendo wameendelea kujiweka sawa kwa kufanya mazoezi makali.

BINGWA wa Olimpiki wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji, Conseslus Kipruto, kashusha mkwara mzito wakati akiendelea kujiandaa kwa mbio za dunia za mwaka huu.

Ikiwa imesalia mwezi mmoja tu kabla ya shindano hilo kuanza kule London, England, wanariadha wazalendo wameendelea kujiweka sawa kwa kufanya mazoezi makali.

Mmoja wa wanaridha hao watakaoiwakilisha Team Kenya huko London ni kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 tu, ambaye ndiye bingwa mtetezi wa Olimpiki katika kitengo cha mbio hizo kwa wanaume.

Sasa Kipruto aliyeweka rekodi mpya ya Olimpiki mwaka jana, kamtangazia Mfalme wa mbio hizo Ezekiel Kemboi kuwa utawala wake umekwisha na ni wakati ampishe naye atawale.

Ezekiel Kemboi anayeelekea kustaafu akiwa na miaka 35, katawala mbio hizo  kwa miaka saba tangu 2009 katika mashindano makubwa ya kidunia akishindwa mara tatu tu 2010 kwenye mbio za Afrika, 2014 kwenye mbio za Madola na mwaka jana alikoshindwa kumaliza mbio hizo.

Kipruto ambaye ana matumaini ya kushinda dhahabu kwa mara nyingine atakapotua London, kawatishia wapinzani wake akiwemo Kemboi kwamba wana kibarua kwa sasa kwa yeyote anayedhania itakuwa rahisi kumbwaga.

“Baada ya kushinda Olimpiki, sasa nina lengo na presha ya kudumisha heshima hiyo. Ninachokusudia kwa sasa ni kuwa Mfalme wa mbio hizi duniani badala ya Kemboi. Hana jinsi, muda wake umekwisha, utawala unaoanza ni wangu,” alisema Kipruto.

Lakini kama ulidhania ni dogo huyo tu mwenye kiburi hicho, basi utahitaji kutega sikio uyasikie ya Geoffrey Kamworor mwenye miaka 24 ambaye naye pia kaapa liwalo na liwe lazima auangushe utawala wa mbabe wa mbio za mita 10,000 Mo Farah kabla hajastaafu mbio hizo.

Kamworor bingwa wa dunia wa nyika ambaye hajawahi kumbwaga Mo Farah hata siku moja, kasema kwamba amelazimika kubadilisha mtindo wake wa ukimbiaji na kawa mjanja zaidi.

“Nimelazimika kubadilisha mbinu zangu za kiufundi na kwa mazoezi ya kutosha kutoka sasa hadi Agosti, nina uhakika wa asilimia 100 kuwa Farah safari hii lazima atalala. Wakati umewadia kwa mwanariadha mzalendo kuirejesha heshima yetu ya zamani katika mita 10,000. Wakati huo ni sasa na nipo tayari,” Kamworor naye kajishaua vile vile.