Kenyatta awabeba mashemeji

Saturday July 1 2017

 

By THOMAS MATIKO

NI mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa kisiasa nchini na sasa kampeni zake zimechaha kwa wanasiasa kupita huku na kule wakiomba kura na kumwaga ahadi lukuki ambapo Rais, Uhuru Kenyatta, anayetetea kiti chake kaahidi kuzifadhili Gor Mahia na AFC Leopards endapo atachaguliwa tena.

Gor na Leopards ndizo klabu kongwe zaidi za soka nchini zikianzia tangu miaka ya uhuru kutoka kwa mkoloni na kila moja inajivunia kuwa na zaidi ya mashabiki milioni sita kote nchini, wengi wakiwa katika ngome zao za kimeneo.

Kwenye Manifesto ya chama chake tawala, Jubilee, iliyozinduliwa siku chache zilizopita, Kenyatta kaahidi kumwaga pesa kuziinua klabu hizo ambazo kufika mwakani hazitakuwa na udhamini baada ya SportPesa kutangaza itajiondoa kuzidhamini, kufuatia hatua ya kiongozi huyo kutia sahihi sheria ya kuitoza kodi ya juu.

Katika Manifesto hiyo, kipengele kinachogusia masuala ya michezo, kinaeleza: “Ndani ya miaka mitano ijayo (kama tukichaguliwa tena), tutasapoti na kuziinua klabu za kitaifa, tutawekeza katika miundo misingi ya kuvikuza timu chipukizi, na pia kufadhili mahitaji mengine yanayotakiwa katika uimarishaji wa talanta za wanamichezo wachipukizi.”

Ahadi hii ya Rais haijaonekana kuwaingia wengi akilini hasa ikizingatiwa kuwa kwenye kampeni za mwaka 2013, Rais Kenyatta aliahidi kujenga viwanja vitano vya kisasa katika miji mikuu nchini, lakini mpaka wa sasa hakuna uwanja aliofanikiwa kuujenga.