Kenya yajipanga kucheza Kombe la Dunia

Wednesday February 28 2018

 

By VINCENT OPIYO

RAIS wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta akilala na kuamka anaota ndoto moja tu! Kwamba siku moja timu ya taifa Harambee Stars itashiriki Kombe la Dunia.

Kenyatta ni mmoja wa marais na mabingwa wa michuano hii waliobahatika kuligusa kombe hili lenye thamani ya Shilingi 1 bilioni ya Kenya kabla ya kuelekea nchini Russia kwa ajili ya fainali za mwaka huu kwanzia Juni.

Juzi Jumatatu, kombe hilo lilitua nchini kutoka Ethiopia na moja kwa moja kuelekea Ikulu ambapo alilibeba Kenyatta kwa mara ya pili kama rais. Mara ya kwanza kombe hili lilitua nchini mwaka 2009 na kubebwa na rais wa wakati huo Mwai Kibaki kabla ya fainali za mwaka 2010 Afrika Kusini na mwaka 2013 Kenyatta akaliinua likielekea nchini Brazil.

“Siku moja hawa wachezaji wetu wataingia uwanjani kushiriki kombe la dunia. Kwa sasa acha tuwashukuru FIFA (Shirikisho la Soka duniani) na kampuni ya Coca Cola kulileta humu nchini kwa mara nyingine tena,” alisema Uhuru.

“Pia, siku ya leo ni muhimu sana na ndio maana tuna baadhi ya magavana hapa kudhibitisha ushirikiano wetu kuendeleza spoti nchini. Kama serikali ya kitaifa tutawapa kila sapoti ili kushirikiana kukuza vipaji kutoka mashinani.”

Kombe hilo juzi Jumanne lilipelekwa katika ukumbi wa kimataifa wa KICC kutizamwa na wananchi na hiyo jana kuelekea nchini Mozambique.

Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa alisema atahakikisha Kenya inafuzu fainali za mwaka 2022 kule Qatar chini ya uongozi wake.