Ivan awashika pabaya Ingwe

Muktasari:

·         Kwa sasa Ingwe iko nafasi ya 10 katika KPL ikiwa imecheza mechi 23, ambazo alisimama kama kocha.

KIMENUKA na hali si shwari tena, Kocha wa zamani wa AFC Leopards, Mbelgiji Ivan Minnaert, ameendelea kushikilia shingo za mabosi wa Ingwe na sasa anadai fidia ya sh. 7 milioni.

Mabosi wa Ingwe wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Dan Mule ulimfuta kazi Minnaert wiki mbili zilizopita kutokana na matokeo mabovu huku ikitangaza kuwa itamlipa fidia ya Sh. 800,000 kulingana na vipengele kwenye mkataba wake.

Kocha huyo alikuwa na mkataba miaka miwili na ambao ulipaswa kumalizika mwakani, lakini Ingwe ikauvunjilia mbali baada ya kuona timu inazidi kuporomoka kwenda chini. Kwa sasa Ingwe iko nafasi ya 10 katika KPL ikiwa imecheza mechi 23, ambazo alisimama kama kocha.

Mawakili wa Minnaert wameitwanga barua kali Ingwe wakitaka ufafanuzi wa kumfuta kazi mteja wao kwani, wanahisi uamuzi uliofanyika haikuziangatia sheria na vipengele kwenye mkataba wake.

Katika barua hiyo, wanasheria hao wanasema usimamizi mbovu wa klabu umechangia matokeo mabovu kwa timu hivyo, wanataka mteja wao arejeshwe kwenye nafasi yake ama alipwe fidia ya Sh. 7 milioni ya kuvunja mkataba wake.

“Mteja wetu anaamini uamuzi wenu wa kumfuta kazi kwa kutumia vipengele  7b na 7c ulibuniwa ili kuhakikisha mnakwepa kumlipa fidia anayostahili pindi mnapotaka kuvunja mkataba. Tunataka mteja wetu arejeshewe wadhifa wake au alipwe Sh7 milioni kama thamani halisi ya kuvunja mkataba wake,” ilisema barua hiyo.

Pia, wanasheria hao wamewataka mabosi wa Ingwe kuendelea kumlipia kodi na kumgharamia usafiri mteja wao hadi pale mkataba wake utakapomalizika.